52. Kuinuka kutoka katika Rukuu´ na du´aa zake


Baada ya hapo alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiuinua mgongo wake kutoka katika Rukuu´ na kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”[1]

Vivyo hivyo alimwamrisha yule mtu aliyeswali vibaya na kumwambia:

“Haitimii swalah ya yeyote mpaka… alete Takbiyr… aende katika Rukuu´… halafu aseme:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

mpaka asimame kwa kunyooka sawasawa.”[2]

Pindi alipokuwa akiinua kichwa chache anasimama na kunyooka sawasawa mpaka kila pingili ya uti imerudi mahala pake[3]. Alikuwa akisema hali ya kuwa amesimama:

رَبَّنَا [وَ]لَكَ الْحَمْدُ

“Ee Mola wetu! [Na] himdi zote ni Zako!”[4]

Amemwamrisha kufanya hivo kila mswaliji akiwemo yule anayeswali nyuma ya imamu na kusema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”[5]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imamu amewekwa ili aweze kufuatwa… na pindi anaposema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

semeni:

اللَّهُمَّ]رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ]

“[Ee Allaah] Mola wetu! Na himdi zote ni Zako.”

Allaah anakusikieni. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”[6]

Amefafanua (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sababu ya kufanya hivo katika Hadiyth nyingine pale aliposema:

“Yule ambaye maneno yake yataafikiana na maneno ya Malaika basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[7]

Wakati wa kuinuka huku akiinyanyua mikono yake kama katika Takbiyrat-ul-Ihraam[8]. Akisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa ni mwenye kusimama:

1-

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako!”[9]

2-

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“Mola wetu! Na himdi zote ni Zako!”[10]

3-

اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

“[Ee Allaah] Mola wetu! Himdi zote ni Zako!”

4-

اللَّهُمَّ رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“[Ee Allaah] Mola wetu! Na himdi zote ni Zako.”[11]

Alikuwa akiamrisha kusema hivo na kusema:

“Pindi imamu anaposema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

semeni:

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako!”

Yule ambaye maneno yake yataafikiana na maneno ya Malaika basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[12]

Mara nyingine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiongezea juu ya hilo na kusema:

5-

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ مِلءَ السَّمَواتِ وَمِلْءَ الأَرْضِ وَمِلْءَ مَا شِئْتَ مِنْ شَيْءٍ بَعْد

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako zimejaa mbingu, ardhi na vyengine vyote Ulivyovitaka baada yake.”[13]

na:

6-

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ مِلءَ السَّمَواتِ وَمِلْءَ الأَرْضِ وَمِلءَ مَا بَيْنَهُمَا وَمِلْءَ مَا شِئْتَ مِنْ شَيْءٍ بَعْد

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako zimejaa mbingu, ardhi, vilivyomo ndani yake na vyengine vyote Ulivyovitaka baada yake.”[14]

Wakati mwingine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiongezea juu ya hilo na kusema:

7-

أَهْلَ الثَّنَاءِ والْمَجْدِ لا مانعَ لما أَعْطَيْتَ وَلا مُعْطِي لما مَنَعْتَ ولا يَنْفَعُ ذَا الجَدِّ مِنْكَ الْجَد

“Wewe ni mstahiki wa kusifiwa na kutukuzwa. Hapana awezaye kukizuia Ulichokitoa na wala hapana awezaye kutoa Ulichokizuia. Wala haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako[15].”[16]

8-

أَهْلَ الثَّنَاءِ والْمَجْدِ أَحَقُّ ما قَالَ الْعَبْدُ وَكلُّنا لَكَ عَبْدٌ اللهمَّ لا مانعَ لما أَعْطَيْتَ وَلا مُعْطِي لما مَنَعْتَ ولا يَنْفَعُ ذَا الجَدِّ مِنْكَ الْجَد

“Wewe ni mstahiki wa kusifiwa na kutukuzwa. Ni ya kweli kabisa aliyoyasema mja Wako. Sote ni Waja Wako. Ee Allaah! Hapana awezaye kukizuia Ulichokitoa na wala hapana awezaye kutoa Ulichokizuia. Wala haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako.”[17]

Mara nyingine anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika swalah ya usiku:

9-

لربي الحمد لربي الحمد

“Himzi zote zinamstahikia Mola wangu. Himzi zote zinamstahikia Mola wangu.”

Akikariri hivo tena na tena mpaka kisimamo chake kinakuwa karibu sawa na urefu wa Rukuu´ yake ambayo ilikuwa karibu ndefu kama kisimamo chake cha kwanza ambapo alisoma ndani yake Suurah “al-Baqarah”[18].

10-

[رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ حمداً كَثِيراً طَيِّبَاً مُبَاركاً فيه [مباركا عليه، كما يحب ربنا و يرضى

“Mola wetu! Na himdi na sifa zote ni Zako, himdi nyingi, nzuri, zenye baraka [zenye baraka juu yake, kama anavyopenda Mola wetu na kuridhia!]”

Kuna mwanamume mmoja aliyekuwa anaswali nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema hivo baada ya kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

Baada ya swalah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni nani aliyesema maneno hayo punde tu?” Mwanaume yule akasema: “Ni mimi, ee Mtume wa Allaah.” Ndipo Mtum wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nimewaona Malaika zaidi ya thelathini wakishindana ni nani atayekuwa wa kwanza kuyaandika.”[19]

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Abu Daawuud na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[3] al-Bukhaariy na Abu Daawuud. Imetajwa katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (722).

[4] al-Bukhaariy na Ahmad.

[5] al-Bukhaariy och Ahmad.

[6] Muslim, Abu ´Awaanah, Ahmad na Abu Daawuud.

Uzinduzi

Hadiyth haithibitishi ya kwamba maamuma hawatakiwi kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

Wala haithibitishi kuwa imamu hatakiwi kusema:

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako!”

baada ya imamu kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

Yanayofahamisha hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema wakati aliposwali kama imamu:

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

“Mola wetu! Himdi zote ni Zako!”

Vilevile Hadiyth:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

inafahamisha kuwa maamuma wanatakiwa kusema kama asemavyo imamu. Kuna ndugu waheshimiwa waliorejea kwangu kuhusu masuala haya. Natarajia watayafikiria hayo, huenda katika yale niliyoyataja kuna yenye kukinaisha. Anayetaka kujua zaidi basi asome kijitabu cha Haafidhw as-Suyuutwiy “Daf´-ut-Tashniy´ fiy Hukm-it-Tasmiy´” kilichoko katika kitabu chake “al-Haawiy lil-Fataawaa” (1/529).

[7] al-Bukhaariy na Muslim. Imesahihishwa na at-Tirmidhiy.

[8] al-Bukhaariy na Muslim. Huku kunyanyua mikono kumepokelewa kupitia njia nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndio maoni ya wanachuoni wengi wakiwemo baadhi ya Hanafiyyah.

[9] al-Bukhaariy na Muslim.

[10] al-Bukhaariy na Muslim.

[11] al-Bukhaariy na Ahmad. Haya aliyasahau Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika ”Zaad-ul-Ma´aad” ambapo akakanusha usahihi wa matamshi:

اللَّهُمَّ رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“[Ee Allaah] Mola wetu! Na himdi zote ni Zako.”

Haya pamoja na kuwa matamshi haya yamepokelewa katika ”as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy, “al-Musnad” ya Ahmad na an-Nasaa´iy kupitia njia mbili kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh), kwa ad-Daarimiy kupitia kwa Ibn ´Umar, kwa al-Bayhaqiy kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy na vilevile kwa an-Nasaa´iy tena kupitia kwa Abu Muusa al-Ash´ariy.

[12] al-Bukhaariy na Muslim. Imesahihishwa na at-Tirmidhiy.

[13] Muslim na Abu ´Awaanah.

[14] Muslim na Abu ´Awaanah.

[15] Utajiri wa kilimwengu kama mali, kizazi, uwezo na nguvu havitoweza kumuokoa kutokamana na Wewe. Kitachomnufaisha na kumuokoa ni matendo mema peke yake.

[16] Muslim na Abu ´Awaanah.

[17] Muslim, Abu ´Awaanah na Abu Daawuud.

[18] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (335).

[19] Maalik, al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 117-120
  • Imechapishwa: 18/02/2017