52. Fadhila za Maswahabah kumi waliobashiriwa Pepo


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

17- Hakika ni kikundi kisichokuwa na shaka yoyote juu yao

     watakuwa juu ya farasi wa kwenye Firdaws kwa nuru wakitembea

18- Sa´iyd, Sa´d, Ibn ´Awf na Twalhah

     ´Aamir Fihr na az-Zubayd wenye kusifiwa

MAELEZO

Hakika ni kikundi… – Kikundi kinachokusudiwa hapa ni watu wasiopungua kumi. Wanaokusudiwa hapa ni wale kumi walioahidiwa Pepo[1].

… juu ya farasi wa kwenye Firdaws… – Bi maana juu ya farasi wa Peponi.

… kwa nuru wakitembea – Wakienda wapendapo.

Pindi alipowataja Maswahabah kumi (Radhiya Allaahu ´anhum) hapa ndipo akawataja wale kumi walioahidiwa Pepo. Wamebaki sita miongoni mwa wale kumi:

Wa kwanza: Sa´iyd. Anaitwa Sa´iyd bin Zayd bin ´Amr bin Nufayl. Ni mtoto wa ami yake ´Umar bin al-Khattwaab. Alikuwa ni mume wa dada yake na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum).

Wa pili: Sa´d. Anaitwa Sa´d bin Abiy Waqqaas az-Zuhriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Wa tatu: Ibn ´Awf. Anaitwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh). Alikuwa ni katika Maswahabah matajiri na miongoni mwa wale ambao wanajitolea sana katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall).

Wa nne: Twalhah. Anaitwa Twalhah bin ´Ubaydillaah (Radhiya Allaahu ´anh).

Wa tano: ´Aamir. Anaitwa Abu ´Ubaydah ´Aamir bin Jarraah (Radhiya Allaahu ´anh). Yeye ndiye mwaminifu wa Ummah huu.

Fihr alikuwa ni katika babuze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na katika mababa wa ma-Quraysh.

Wa sita: az-Zubayr. Anaitwa az-Zubayr bin ´Awwaam (Radhiya Allaahu ´anh). Alikuwa ni msaidizi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Hawa sita, pamoja na wale makhaliyfah wanne, wanakuwa kumi waliobashiriwa Pepo. Wao ndio Maswahabah bora. Wote wanatokamana na kabila la Quraysh.

[1] Abu Daawuud (4650) na (4649), at-Tirmidhiy (3757) na (3748), an-Nasaa´iy (1630), Ibn Maajah (134), Ahmad (01/187-188) na wengineo.