51. Tunapenda waja wema lakini ni haramu kuwaabudu pamoja na Allaah

Hapana shaka kwamba maiti si kama aliyehai. Aliyehai anaweza kutembea, anaweza kula, anaweza kunywa, anaweza kuchuma na anaweza kufanya matendo. Kuhusu maiti matendo yake yamekatika. Vipi basi wakifa wanafanywa kuwa waungu badala ya Allaah (´Azza wa Jall) ilihali wao ni wafu na hawamiliki chochote hata juu ya nafsi zao wenyewe? Hawezi hata kujifanyia kitu juu ya nafsi yake mwenyewe. Vipi basi mtu atamtegemea na akawaomba haja mbalimbali ilihali hana kitu na si muweza? Lakini maumbile yakiharibika, watu wanafuata kibubusa na mashaytwan wanawapambia watu mambo haya. Bali wao wanaita mambo haya kuwa eti ndio Tawhiyd na wanaita Tawhiyd kuwa ndio kufuru na shirki. Wanawaambia wale wanaowakaripia kwamba eti hawawapendi mawalii kwa kuwa hawawaombi,  hawawachinjii na hawawawekei nadhiri. wanasema kuwa ni kuwachukia. Kwa mujibu wao mtu kuwapenda mawalii ni yeye awafanye kuwa washirika na waungu badala ya Allaah!

Ndio, sisi tunawapenda mawalii wa Allaah sawa waliohai na waliokufa. Tunawapenda, tunawaiga na tunawaombea du´aa. Ama kusema eti sisi tuwafanye kuwa ni washirika pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na tujikurubishe kwao kwa kufanyia ´ibaadah, huku sio kuwapenda waja wema. Kwa kuwa watu wema wenyewe hawaridhii shirki na hawaridhii wao kuabudiwa pamoja na Allaah (´Azza wa Jall). Hivyo, ni nani anayewapenda watu wema? Mshirikina au mpwekeshaji? Bila ya shaka ni mpwekeshaji ndio anawapenda watu wema, kuwafanya ni marafiki, anawaombea, anawaiga na anawaombea msamaha. Huyu ndiye anawapenda watu wema na si yule anayewaomba badala ya Allaah na kuwachinjia na kuwawekea nadhiri. Wao hawaridhii hili na wala hawamiliki katika dini hii lolote na wewe umewapandisha hadhi na nafasi wasiostahiki. Wewe lau utamwendea mmoja katika watu wa kawaida na kumwambia: “Wewe ni kama mfalme au wewe ni mfalme kabisa”. Je, mtu huyu si atachukulia kuwa unamfanyia maskhara kwa sababu umempandisha manzilah ambayo hakuifikia. Kwa hiyo yule anayewapandisha waja wema katika manzilah ya Allaah, basi huyu kwa hakika amewatukana na kuwadharau na wala hawapendi. Anayewapenda ni yule ambaye anawaigiza na anawaombea.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 06/09/2018