Swali 51: Watu wengi hawaswali isipokuwa swalah ya ijumaa peke yake na nyakati za Ramadhaan peke yake na wanajengea hoja Hadiyth isemayo:

“Swalah ya ijumaa moja mpaka swalah ya ijumaa nyingine na Ramadhaan moja mpaka Ramadhaan nyingine ni kifutio cha madhambi kwa yaliyo kati yake.”

Je, kitendo hichi ni sahihi[1]?

Jibu: Kujengea hoja huku ni ujinga na upotofu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ametuwajibishia swalah tano, ametuwajibishia swalah ya ijumaa na ametuwajibishia kufunga Ramadhaan. Kwa hivyo ni lazima kwetu kutekeleza yale mambo ya wajibu yote na kutatadhari na yale ambayo Allaah ametuharamishia. Hiyo ina maana kwamba tunatakiwa kutekeleza swalah zote na tutekeleze swalah ya ijumaa. Aidha tufunge Ramadhaan, tuhiji Nyumba na tufanye yale yote ambayo Allaah ametuwajibishia na tujichunge na yale ambayo Allaah ametukataza hali ya kuwa ni wenye kutaraji thawabu na kuchelea adhabu Yake. Kwa kufanya hivo tutapata ujira mkubwa na mwisho mwema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), katika Hadiyth hiyohiyo aliyoitaja, amezindua jambo kwa kusema:

“Swalah tano, swalah ya ijumaa moja mpaka swalah ya ijumaa nyingine na Ramadhaan moja mpaka Ramadhaan nyingine ni kifutio cha madhambi kwa yaliyo kati yake muda wa kuwa mtu atajiepusha na madhambi makubwa.”[2]

Akabainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba ´ibaadah hizi zinakuwa ni kama kifutio kwa yalio kati yake ambayo ni yale madhambi madogomadogo muda wa kuwa mtu anajiepusha na madhambi makubwa. Haya yanabainisha ubatilifu wa yale aliyofikiri muulizaji na yale aliyoyapangia Allaah katika kafara. Aidha linaweka wazi kwamba ´ibaadah hizi zinakuwa ni kifutio cha madhambi kwa yalio kati yake kwa yule ambaye atatekeleza mambo ya faradhi na akajiepusha na madhambi makubwa. Yanayojulisha maana hii ni maneno ya Allaah (Subhaanah):

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Endapo mtajiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa, basi Tutakufutieni madhambi yenu madogo na tutakuingizeni katika mahali patukufu.”?[3]

Akabainisha (Subhaanah) katika Aayah hii kwamba kufutwa kwa makosa na kuingia Peponi ni jambo limefungamanishwa na kuyaepuka madhambi makubwa. Madhambi makubwa ni yale maasi ambayo kwa mujibu wa maandiko yametajwa sambamba na kutishiwa laana, Moto, kupatwa na ghadhabu za Allaah, kukanushwa imani ya yule mtendaji, Allaah au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kujitenga naye mbali na mfano wake mambo ambayo yanafahamisha ukubwa na ukhatari wake. Kwa mfano amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah amemlaani mwizi ambaye anaiba yai akakatwa mkono wake na akaiba kamba akakatwa mkono wake.”[4]

Vilevile amemlaani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mnywaji pombe, mbebaji, mwenye kuitengeneza, kifaa kinachoibeba, mwenye kuiuza na anayekula thamani yake. Mfano mwingine amemlaani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mla ribaa, mwakilishi wake, mwandishi wake na shahidi wake. Mfano mwingine amemlaani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwenye kufanya chanjo na mwenye kufanywa chanjo, mwenye kuchonga nyusi na mwenye kuchongwa nyusi na mwenye kufanya mwanya kwa ajili ya kutafuta urembo wanaoyabadilisha maumbile ya Allaah. Mfano mwingine ni pale aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini na wala hanywi pombe pale anapokunywa hali ya kuwa ni muumini.”[5]

Mfano mwingine ni pale aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi najitenga mbali na anayeomboleza, anayenyoa nywele na mwenye kupasua nguo.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Anayeomboleza ni yule anayenyanyua sauti yake wakati wa msiba. Mwenye kunyoa nywele zake ni yule anayefanya hivo wakati anapopata msiba. Mwenye kupasua nguo ni yule anayepasua nguo yake kipindi cha msiba.

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Waislamu wote wameafikiana kwamba kufunga Ramadhaan hakudondoshi mambo ya wajibu mengine kutoka kwa waislamu kama ambavo swalah ya ijumaa pia haiondondoshi mambo ya wajibu mengine na kwamba swalah ya ijumaa haidondoshi swalah nyenginezo za wajibu. Swalah ya ijumaa inadondosha swalah ya Dhuhr peke yake katika ile siku ya ijumaa.

Yeyote atakayedai kwamba swalah ya ijumaa na kufunga Ramadhaan kunadondosha kutoka kwake faradhi hizi zote na akaamini hivi, basi huo ni ukafiri na upotofu kwa mujibu wa wanazuoni wote. Ni lazima kwa aliyesema hivo kufanya haraka kutubu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kufanya hivi ni kuyaondodosha mambo ya wajibu na kuyahalalisha yaliyo ya haramu, mambo ambayo ndio kipeo cha ukafiri na upotofu. Aidha ni kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu. Tunamwomba Allaah usalama na afya kutokamana na hayo.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/419).

[2] Muslim (342) na Ahmad (8830) na tamko ni lake.

[3] 4:31

[4] al-Bukhaariy (6301) na Muslim (3195).

[5] al-Bukhaariy (2475) na (5578) na tamko ni lake na Muslim (57).

[6] al-Bukhaariy (1296) na Muslim (104).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 101-104
  • Imechapishwa: 09/12/2021