50- Inajuzu kutembea mbele ya jeneza na nyuma yake, upande wa kuliani mwake na kushotoni mwake muda wakuwa yuko karibu nalo. Isipokuwa ikiwa mtu amepanda kipandwa ndiye ambaye atatembea nyuma yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mpandaji [atatembea] nyuma ya jeneza na mwenye kutembea kwa miguu atakapo. [Nyuma yake, mbele yake, kuumeni kwake na kushotoni kwake hali ya kuwa karibu nalo]. Kipomoko kinaswaliwa. [Wazazi wake wataombewa msamaha na rehema].”

Ameipokea Abu Daawuud (02/65), an-Nasaa´iy (01/275-276), at-Tirmidhiy (02/144), Ibn Maajah (01/451, 458), at-Twahaawiy (01/278), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (769), al-Bayhaqiy (84, 25), at-Twayaalisiy (701-702), Ahmad (04/247, 248-249, 252) kupitia kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Mambo ni kama alivosema.

Mtiririko ni wa an-Nasaa´iy na Ahmad katika moja ya mapokezi.

Upokezi wa tatu ni wa Abu Daawuud, al-Haakim na at-Twayaalisiy. Ahmad ana zile za mwanzo katika hizo na al-Bayhaqiy hiyo ya tatu.

Abu Daawuud na Ibn Hibbaan wamesema:

“Kipomoko” badala ya “mtoto” na ni upokezi wa al-Haakim, al-Bayhaqiy na Ahmad. al-Haafidhw ameiegemeza katika “at-Talkhiysw” (05/147) na pia kwa at-Tirmidhiy, jambo ambalo ni kosa. Tamko lililoko kwake ni kama lile lilioko kwa wanachuoni wengi.

51- Yote mawili katika kutembea kwa mbele na kwa nyuma yake yamethibiti kufanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuhusu hilo:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr na ´Umar walikuwa wakitembea mbele na nyuma ya jeneza.”

Ameipokea Ibn Maajah (1483) na at-Twahaawiy (01/278) kupitia njia mbili kutoka kwa Yuunus bin Yaziyd kutoka kwa Ibn Shihaab ambaye naye amepokea kutoka kwake.

Cheni ya wapokezi hii ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim[1].

51- Lakini bora ni kutembea kwa nyuma yake. Kwa sababu ndivo yanavopelekea maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na yafuateni majeneza… “

na mengine yaliyo na maana kama hiyo katika yale yaliyotanguli katika masuala ya 43 mwanzoni mwa kipengele hichi. Isitoshe yanatiliwa nguvu na maneno ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kutembelea nyuma yake ndio bora kuliko kutembea mbele yake kama mfano wa swalah ya anayeswali katika mkusanyiko juu ya anayeswali peke yake.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (04/101), at-Twahaawiy (01/279), al-Bayhaqiy (04/259), Ahmad (754). Pia ameipokea Ibn Hazm katika “al-Muhallaa” (05/165) na Sa´iyd bin Mansuur kupitia njia mbili kutoka kwake. al-Haafidhw amesema (03/143) katika moja ya hayo mawili:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Imesimamia kwake yeye Swahabah lakini yakiwa na hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini al-Athram amesimulia kutoka kwa Ahmad kwamba amezungumzia kwa kuitia dosari cheni ya wapokezi wake.”

Lakini inapata nguvu kwa njia nyingine.

Tanbihi!

ash-Shawkaniy amesema baada ya maneno yake yaliyotangulia:

“Ameeleza mtunzi wa “al-Bahr”, kutoka kwa ath-Thawriy kwamba amesema:

“Aliyepanda kipando atatembea nyuma ya jeneza na mwenye kutembea kwa miguu mbele yake. Aliyoyasema yanafahamishwa na Hadiyth ya al-Mughiyrah iliyotangulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Aliyepanda kipando atakuwa nyuma ya jeneza na mwenye kutembea kwa miguu atakuwa kwa mbele yake karibu nalo kuliani kwake au kushotoni kwake.

Wameipokea watunzi wa “as-Sunan” na ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hibbaan na al-Haakim. Haya ni madhehebu yenye nguvu… “

Hapana sivyo hivyo. Hadiyth yenye matamshi kama haya imepokelewa na Ahmad kupitia kwa al-Mubaarak bin Fadhwaalah. Ndani yake kuna udhaifu. Kuna mwingine amezidisha ambapo akasema:

“… kwa nyuma na kwa mbele yake… “

Kama ilivyotangulia kuashiriwa. Ameipokea al-Mubaarak pia kwa at-Twayaalisiy. Kwa hiyo ni lazima kuitendea kazi. Ni dalili katika kutoa khiyari na si kuonyesha kuwa bora ni kutangulia mbele yake.

Miongoni mwa mambo yanayoshangaza ni kwamba ziada hii ameitaja mtunzi wa “al-Muntaqaa´” katika maeneo yaliyoashiriwa na ash-Shawkaaniy hapo punde tu kisha akaghafilika nayo.

[1] Kuhusiana na yale yaliyoko katika ”al-Jawhar-un-Naqiyy” (04/25):

”Katika ”al-Muswannaf” ya ´Abd-ur-Razzaq, kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Twaawuus, kutoka kwa baba yake aliyesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupatapo kutembea isipokuwa nyuma ya jeneza mpaka nilipokufa.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za wanachuoni.”

Itakuweje hivo ilihali Hadiyth hiyo ni Mursal? Hakika Twaawuus alikuwa ni Taabi´iy na yeye amepokea moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth ambayo ni Mursal sio hoja kwa mujibu wao. Isitoshe imepingana na Hadiyth ya Anas ambayo ni Swahiyh. ash-Shawkaaniy (04/62) pia ameitia dosari ya Irsaal. Lakini hata hivyo alisema:

”Sijawahi kuiona katika chochote katika vitabu vya Hadiyth.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 94-96
  • Imechapishwa: 08/07/2020