51. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Allaah ana majina mazuri mno; hivyo basi muombeni kwayo”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلّهِ الأَسْمَاء الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno; hivyo basi muombeni kwayo na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake. Watalipwa yale waliokuwa wakifanya.” (al-A´raaf 07:180)

Ibn Abiy Haatim amepokea kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema kuhusu:

وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ

“… na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake.”

“Wanashirikisha.”

Amesema vilevile:

 “Wametoa jina la al-Laat kutoka katika al-Ilaah na al-´Uzzaa kutoka katika al-´Aziyz.”

2- al-A´mash amesema:

“Wameingiza ndani yake yasiyokuwemo.”

MAELEZO

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلّهِ الأَسْمَاء الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno; basi muombeni kwayo na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake. Watalipwa yale waliokuwa wakifanya.”

Allaah (Ta´ala) amebainisha kwamba ana majina mazuri mno ambayo hayawezi kuingiwa na upungufu wowote. Yote ni majina kamilifu na ni yenye kujulisha maana tukufu. Allaah anasifika nayo kwa njia inayolingana Naye. Anatakiwa kuombwa kwayo kwa mfano kwa kusema “Ewe Mwingi wa huruma, ewe Mwenye nguvu kabisa, ewe Mwenye kughufuria, nisamehe” na kadhalika.

Kuyapotoa majina Yake maana yake ni kupondoka kutoka katika haki na kumshirikisha na kuyatumia kwa mwingine asiyekuwa Allaah. Kama ambavyo mtu anamwabudu mwingine asiyekuwa Allaah na hivyo akawa kafiri kwa ajili ya hilo. Kadhalika inahusiana na yule mwenye kuyapotoa majina Yake kwa kupondoka kutoka katika haki na akasema kuwa hayana maana. Kama walivofanya Jahmiyyah, ambao wamekanusha sifa na majina ya Allaah, na Mu´tazilah, ambao wamekanusha sifa Zake. Wameyapotoa majina na sifa Zake na kwa kukengeuka kutoka katika haki.

Kuna aina mbili za kuyapotoa:

Upotoshaji mkubwa: Ni jambo linawatumbukiza katika kufuru.

Upotoshaji mdogo: Ni jambo wanatumbukia ndani yake baadhi ya waislamu pale wanapokosa kujisalimisha katika haki kikamilifu. Kwa njia hiyo wanakuwa ni wenye kukosa Uislamu na imani kamilifu kwa kiasi cha upotoaji wao na kupondoka kwao kutokamana na haki.

2- al-A´mash amesema:

“Wameingiza ndani yake yasiyokuwemo.”

Hii ni aina fulani ya upotoaji, nako ni kule kumwita Allaah kwa majina ambayo hakuyateremshia dalili yoyote. Hii ni aina fulani ya upotoaji na batili.

Upotoaji mwingine ni kusema al-Laat kutoka katika al-Ilaah na al-´Uzzaa kutoka katika al-´Aziyz.

Kadhalika kuingia katika maasi ni aina fulani ya upotoaji mdogo. Mwenye kumkanusha Allaah au akamshirikisha Allaah na mwingine ametumbukia katika upotoaji mkubwa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 151
  • Imechapishwa: 06/11/2018