51. Kila muislamu anatakiwa kuswaliwa swalah ya jeneza


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Swalah ya jeneza anaswaliwa muislamu aliyekuwa akimpwekesha Allaah. Huyu anaombewa msamaha. Hatakiwi kunyimwa hilo. Wala haitakiwi kuacha kumswalia kutokana na dhambi aliyotenda, sawa iwe kubwa au ndogo. Jambo lake liko kwa Allaah (Ta´ala).”

MAELEZO

Kwa sababu kila mwenye kumpwekesha Allaah kunatarajiwa juu yake kuingia Peponi hata kama ataadhibiwa ataanza kwanza kuadhibiwa Motoni. Haifai kwetu kuwakufurisha waislamu wenye kutenda madhambi makubwa. Bali ni wajibu kwetu kuamini kwamba kila ambaye alikuwa akimwabudu Allaah pekee, mwenye kuswali swalah vipindi vitano na ni mwenye kujiepusha na yale mambo yote yanayochengua Uislamu, basi hukumu yake ni kama hukumu ya waislamu wengine wote. Anatakiwa kuswaliwa swalah ya jeneza pindi anapokufa, jeneza lao linatakiwa kufuatwa na kuombewa msamaha. Tunatarajia kwake kuingia Peponi na tunakhofu juu yake kutokana na madhambi yake. Pasi na kujali ni dhambi gani atafanya bado anazingatiwa ni muislamu midhali si mwenye kuonelea kuwa dhambi hiyo ni halali. Atataamiliwa kwa mujibu wa madhambi yake makubwa na jambo lake anaachiwa Allaah; akitaka kumsamehe atamsamehe na akitaka kumuadhibu atamuadhibu kisha baadaye ataingizwa Peponi baada ya kumsafisha kutokana na madhambi yake aliyofanya.

Jengine ni kwamba tunatakiwia kupambanua yale yanayopelekea katika kufuru, nayo ni shirki kubwa, kukanusha nguzo moja wapo miongoni mwa nguzo za Uislamu au nguzo za imani, kuhalalisha kitu ambacho kuna maafikiano juu ya uharamu wake au kuharamisha kitu ambacho kuna maafikiano juu ya uhalali wake. Yote haya yanapelekea katika kufuru. Kadhalika kukifanyia utani Kitabu na Shari´ah ya Allaah, kuchezea shere hukumu ya Kishari´ah au kuacha swalah. Yote haya yanazingatiwa ni miongoni mwa mambo yanayochengua Uislamu wa mtu na kumpelekea yule mwenye kuyafanya na kuyaamini kuwa kafiri.

Mwanafunzi anatakiwa kutahadhari asiyachanganye mambo haya na kutokuweza kupambanua kati ya kufuru kubwa na kufuru ndogo na kati ya shirki kubwa na shirki ndogo. Akiyachanganya mambo haya basi atatumbukia katika Takfiyr kwa njia asiyoihisi. Mwanafunzi anatakiwa kutofautisha kati ya mambo haya mawili ili mambo yote yawe wazi. Anatakiwa kutambua kufuru kubwa ni ipi na kufuru ndogo ni ipi, unafiki mkubwa ni upi na unafiki mdogo ni upi, shirki kubwa ni ipi na shirki ndogo ni ipi.

Mafanikio yote yako kwa Allaah. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 171-172
  • Imechapishwa: 10/06/2019