51. Jihaad ni yenye kuendelea pamoja na kiongozi mwema na muovu mpaka siku ya Qiyaamah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Vita ni vyenye kuendelea pamoja na viongozi wema na waovu mpaka siku ya Qiyaamah na haitakiwi kuachwa. Kiongozi kugawa fai na kusimamisha adhabu ni mambo yenye kuendelea. Hakuna yeyote aliye na haki ya kuwaponda wala kupambana nao. Inafaa na ni sahihi kuwapa zakaah sawa wakiwa wema au waovu. Swalah ya ijumaa nyuma yao na nyuma ya magavana wao inafaa na ni timilifu na ni Rak´ah mbili. Yule mwenye kuirudi ni mtu wa Bid´ah mwenye kuyaacha mapokezi na anaenda kinyume na Sunnah. Hapati chochote katika fadhila za ijumaa midhali haonelei kuwa ni sahihi kuswali swalah ya ijumaa nyuma ya viongozi sawa wawe wema au waovu. Sunnah ni kuswali Rak´ah mbili pamoja nao na kuonelea kuwa ni timilifu. Usiwe na shaka kwenye kifua chako juu ya hilo.”

Midhali Jihaad ni yenye kuendelea mpaka siku ya Qiyaamah basi ni wajibu kupigana chini ya bendera ya kiongozi. Ni mamoja akawa mwema au muovu. Hivyo ndivyo walivyofanya Salaf akiwemo Ibn-ul-Mubaarak, al-Awzaa´iy na Ahmad bin Hanbal. Walikuwa wakitoka kwenda mipakani na wakipambana chini ya uongozi wa ´Abbaasiyyah.

Imaam Ahmad amesema:

“Kiongozi kugawa fai na kusimamisha adhabu ni mambo yenye kuendelea.”

Wanaonelea kuwa viongozi ndio wanaogawa fai na ndio wanaosimamisha adhabu kama vile uzinzi, mauaji, wizi, unywaji pombe na mfano wa hayo. Hii ni kazi ya watawala na sio kazi ya mtu mmoja mmoja wala makundi. Hii ni kazi inayofanywa na mtawala kwa kuwa ni haki yake. Mtu mmoja mmoja na makundi kushikilia jambo hili inapelekea kumwaga damu na mitihani isiyoepukika. Pindi mtawala anaposimamia kazi hii, ingawa ni mtenda dhambi, watu watatulia na Ummah hautawekwa katika mitihani.

Imaam Ahmad amesema:

“Hakuna yeyote aliye na haki ya kuwaponda wala kupambana nao.”

Si katika hiyo adhabu aliyosimamisha wala fai aliyogawa, tofauti na alivyofanya Dhul-Khuwaysirah.

Imaam Ahmad amesema:

“Inafaa na ni sahihi kuwapa zakaah sawa wakiwa wema au waovu.”

Kwa sababu mtawala wa Kiislamu anayo haki ya kugawa fai vile anavyodhani kuwa ni sawa. Madhehebu ya Imaam Ahmad na madhehebu ya Imaam ash-Shaafi´iy wanatofautisha kati ya zakaah ya dhahiri na zakaah iliyojificha. Wanaona kuwa zakaah ya dhahiri anapewa mtawala na zakaah iliyojificha, kama vile dhahabu, fedha na bidhaa za biashara, inatolewa moja kwa moja na yule mmiliki. Wapo wengine wanafadhilisha mtu aitoe kivyake ili kuhakikisha imewafikia wale wenye kuiistahiki. Lakini lau akipewa mtawala ni sahihi. Ikiwa mtawala atataka apewe nayo yeye basi ni lazima kwa wananchi kumtii. Ikiwa watakataa kumpa nayo basi anatakiwa kupambana nao vita kama ambavyo Maswahabah walipambana na wale waliokataa kutoa zakaah.

Imaam Ahmad amesema:

“Swalah ya ijumaa nyuma yao na nyuma ya magavana wao inafaa na ni timilifu na ni Rak´ah mbili.”

Swalah ya ijumaa inatakiwa kuswaliwa nyuma ya kiongozi na nyuma ya wale magavana, mahakimu na maimamu wa misikiti aliowateua. Swalah ya ijumaa nyuma yao inajuzu na ni kamilifu na ni Rak´ah mbili.

Imaam Ahmad amesema:

“Yule mwenye kuirudi ni mtu wa Bid´ah mwenye kuyaacha mapokezi na anaenda kinyume na Sunnah.”

Baadhi ya watu wanairudi swalah ya ijumaa kwa sababu ya kitu wanachoona kuwa ni udhuru. Ima kwa sababu mkusanyiko haukutimia watu arubaini au kwa sababu wanaona kuwa swalah yao nyuma ya imamu sio sahihi. Sababu hii ya pili ni ya khatari zaidi kuliko hiyo ya kwanza. Mtu huyu ni mzushi. Hutakiwi kuirudi swalah hata kama imamu uliyeswali nyuma yake ni mzushi. Swali na wala usiirudi. Vivyo hivyo ikiwa imamu ni mwenye kudhulumu. Swali nyuma yake na wala usiirudi swalah. Ukiirudi swalah ya ijumaa basi wewe ni mzushi.  Imaam Ahmad amesema:

“Sunnah ni kuswali Rak´ah mbili pamoja nao na kuonelea kuwa ni timilifu. Usiwe na shaka kwenye kifua chako juu ya hilo.”

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 422-424
  • Imechapishwa: 02/12/2017