51. Baadhi ya fadhila za ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh)


Amesema mwandishi (Rahimahu Allaah):

16- Wanne wao ni kiumbe bora anaye kuja baada yao

     ´Aliy kiongozi mwema kwa kheri

MAELEZO

Anayefuata baada ya ´Uthmaan katika ubora ni kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib. Ni mtoto wa ami yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mume wa msichana wake Faatwimah ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Je, huridhii kwangu uwe na manzilah kama Haaruun aliokuwa nayo kwa Muusa pamoja na kuwa hakuna Nabii mwingine baada yangu.”[1]

Hapa ilikuwa katika vita vya Tabuuk. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomwacha al-Madiynah akahisi uzito wa kubakia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkinaisha na kumwambia:

“Wewe kwangu manzilah yako ni kama Haaruun aliokuwa nayo kwa Muusa.”

Kwa sababu Muusa alipoenda kwenye miadi ya Mola Wake alimwachia usimamizi Haaruun. Amesema:

اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي

“Shika mahali pangu.” (07:142)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwachia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ashike mahali pake nafasi. Haina maana kwamba yeye ndiye khaliyfah baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama wanavyosema Raafidhwah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya pamoja na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alipoenda katika Tabuuk kama jinsi alivyofanya Muusa pamoja na Haaruun (´alayhimaas-Salaam) alipoenda katika miadi ya Mola Wake. Amesema (Ta´ala):

وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ

“Muusa akasema [kumwambia] ndugu yake Haaruun: “Shika mahali pangu katika [kuwasimamia] watu wangu na tengeneza na wala usifuate njia ya mafisadi.”” (07:142)

Hii ni moja katika fadhila zake (Radhiya Allaahu ´anh).

Yeye ndiye ambaye vilevile aliwapiga vita Khawaarij na akazuia fitina yao na waislamu wakastarehe na shari yao. Hivyo ikawa imepatikana kwake bishara ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kuwapiga vita.

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye kijana aliye huru wa kwanza kusilimu. Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye mwanaume aliye huru wa kwanza kusilimu. Zayd bin Haarith (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye mtu wa kwanza aliyeachwa huru aliyesilimu. Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye mtumwa wa kwanza kusilimu. Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ´anhaa) ndiye mwanamke wa kwanza kusilimu.

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ni katika wale wa awali waliotangulia kuingia katika Uislamu. Mke wake ni msichana wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni Faatwimah. Anaitwa Abul-Hasanayn; al-Hasan bin ´Aliy na al-Husayn bin ´Aliy (Radhiya Alolaahu ´anhumaa) ambao ndio viongozi wa vijana wa Peponi. Ana fadhila nyingi.

Yeye ndiye ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema juu yake siku ya Khaybar:

“Nitampa bendera hii mwanaume anayempenda Allaah na Mtume Wake na Allaah na Mtume Wake nao wanampenda.”[2]

Maswahabah walikuwa wanavizia na kila mmoja akawa anataka yeye ndiye awe mtu huyu ambaye anampenda Allaah na Mtume Wake na Allaah na Mtume Wake nao pia wanampenda. Ikawa si mwingine ni ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Hii ni moja ya fadhila zake kubwa – Allaah awawie radhi wote.

[1] al-Bukhaariy (3706) na (4416) na Muslim (2404) na (32)

[2] al-Bukhaariy (3009) na (3701) na (4210) na Muslim (2406) na (34)