Swali: Yamekuwa mengi maneno ya watu na wametofautiana ni wapi lipo kaburi la bwana al-Husayn. Je, waislamu wanafaidika kujua mahala pake kwa kulengesha?

Jibu: Uhakika wa mambo ni kwamba watu wametofautiana juu ya hilo. Imesemekana kwamba alizikwa Shaam. Imesemekana pia kwamba ni ´Iraaq. Allaah ndiye mjuzi zaidi wa ukweli wa mambo. Kuhusu kichwa chake wametofautiana pia. Imesemakana kwamba ni Shaam. Wengine wakasema ´Iraaq. Wengine wakasema Misri. Maoni ya sawa ni kwamba lile lilioko Misri sio kaburi lake. Ni kosa na huko hakuna kichwa cha al-Husayn.

Baadhi ya wanachuoni wametunga tungo juu ya jambo hilo na wakabainisha kwamba hakuna msingi wa uwepo kichwa chake Misri na wala hakuna mtazamo wa jambo hilo. Lililo na nguvu zaidi ni kwamba kiko Shaam. Kwa sababu alihamishwa kupelekwa kwa Yaziyd bin Mu´aawiyah ambaye alikuwa Shaam. Hakuna mtazamo wa maoni yanayosema kuwa alihamishwa kupelekwa Misri. Kwa hiyo ima alihifadhiwa Shaam katika depo za Shaam au mwili wake ulirudishwa ´Iraaq.

Vovyote itavokuwa watu hawana haja ya kujua ni wapi alizikwa na yuko wapi. Kilichosuniwa ni kumuombea du´aa na rehema. Allaah amsamehe na amridhie. Aliuliwa hali ya kudhulumiwa. Kwa hiyo aombewe msamaha na rehema. Kunatarajiwa juu yake kheri nyingi. Yeye na nduguye al-Hasan ndio viongozi wa vijana wa Peponi. Hayo yamesemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Allaah amewawia radhi wawili hao nao wako radhi Naye. Yule atakayejua lilipo kaburi lake ambapo akamtolea salamu na kumuombea du´aa ni sawa. Ni kama yanavyotembelewa makaburi mengine. Yafanyike hayo bila kuchupa mpaka kwake wala kumfanyia ´ibaadah.

Haijuzu kuomba uombezi kutoka kwake wala kutoka kwa mwengine yeyote kama ilivo kwa wafu wote. Kwa sababu maiti hakuombwi kitu kutoka kwake. Anaombewa du´aa na anatakiwa rehema akiwa ni muislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[1]

Kwa hiyo yule mwenye kulitembelea kaburi la al-Husayn, al-Hasan au wengineo katika waislamu basi wanaombewa rehema na msamaha kama inavyofanywa juu makaburi ya waislamu wengine wote. Hii ndio Sunnah.

Ama kuyatembelea makaburi kwa ajili ya kuwaomba wenye nayo, kuwataka msaada au kuwataka uombezi ni maovu. Bali ni shirki kubwa. Haijuzu kujenga juu ya makaburi msikiti, kuba wala kitu kingine. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.” [2]

Kuna maafikiano juu yake.

Pia Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amepokea katika “as-Swahiyh” kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulitia chokaa kaburi, kuliikalia na kulijengea. Kwa hivyo haijuzu kuyatia chokaa, udongo, kuyawekea sitara au kuyajengea makaburi. Yote haya yamekatazwa na ni katika njia zinazopelekea katika shirki. Hakuswaliwi karibu na makaburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Jundub bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh).

Hadiyth hii inajulisha kwamba haijuzu kuswali kwenye makaburi wala kuyafanya ni mahala pa kuswalia. Jengine ni kwa sababu kitendo hicho ni njia inayopelekea katika shirki au yakaabudiwa badala ya Allaah kwa kuyaomba, kuyataka uokozi, kuyawekea nadhiri au kuyapapasa makaburi yao kwa ajili ya kutafuta baraka. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaonya juu ya hilo. Makaburi yanatembelewa matembezi yanayokubalika kwa misingi ya Shari´ah peke yake, kuyatolea salamu, kuyaombea du´aa na rehema pasi na kufunga safari kwa ajili ya jambo hilo.

MWISHO!

[1] Muslim (976).

[2] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[3] Muslim (532).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 144-147
  • Imechapishwa: 27/07/2022