50. Kufanya sababu hakupingani na kumtegemea Allaah

Kwa hiyo kutegemea ni ´ibaadah kubwa. Nako ni kule kumtegemea Allaah (Jalla wa ´Alaa) na kumwachia mambo yako Yeye. Hili halipingani na mtu kufanya sababu zinazofaa. Akusanye baina ya mambo mawili, afanye sababu zinazojuzu na amtegemee Allaah. Asimtegemee Allaah peke yake na akaacha kufanya sababu zinazofaa na wala asizitegemee sababu peke yake na akaacha kumtegemea Allaah. Bali anatakiwa kukusanya baina ya mambo yote mawili. Namna hii ndivo anavyokuwa muumini.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ndiye mtegemezi mkubwa. Lakini pamoja na haya yote alikuwa akifanya sababu. Alikuwa akiandaa nguvu kwa sababu ya Jihaad. Alikuwa akivaa mavazi ya ngao wakati wa Jihaad. Huku ni kufanya sababu zinazofaa. Muumini anatakiwa kukusanya yote mawili. Afanye sababu zinazofaa pamoja na kumtegemea Allaah. Kwa ajili hii wamesema:

“Kuitegemea sababu pekee ni shirki. Kutokufanya sababu ni kuitukana Shari´ah.”

Kwa sababu Shari´ah imeamrisha mtu kufanya sababu zinazofaa.

Watu hawa – yaani washirikina – wanawategemea wafu, miti na mawe. Wanawategemea viumbe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kukitegemea kitu basi huning´inizwa kwacho.”[1]

Atakayemtegemea Allaah, basi Allaah atamtosheleza. Na yule atakayemtegemea asiyekuwa Allaah, basi hakika Allaah atamwacha kwa hicho kiumbe dhaifu na hatimaye apotee. Kwa sababu kategemea kitu ambacho hakifai kutegemewa. Amemtegemea dhaifu mfano wake au pengine akawa ni dhaifu kuliko yeye.

[1](Kaipokea Ahmad (18781)), (at-Tirmidhiy (2072), (al-Haakim (3/216) na kaifanya kuwa Hasan.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 74
  • Imechapishwa: 04/09/2018