49- Ni lazima kufanya haraka kutembea nalo utembeaji uliochini ya kupiga matiti. Kumepokelewa Hadiyth zifuatazo juu ya hilo:

Ya kwanza: “Fanyeni haraka kumwandaa maiti. Akiwa ni mwema basi ni kheri mnazomtangulizia. Akiwa hayuko hivo ni shari mnayoitua kutoka shingo zenu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na mtiririko ni wa Muslim, watunzi wa “as-Sunan” wane. Ni Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na Ahmad (02/240, 280, 488), al-Bayhaqiy (04/21) kupitia njia ya Abu Hurayrah. Anayo Hadiyth nyingine mfano wake inayofuata:

Ya pili: “Anapobebwa maiti na wanaume wakambeba mashingoni mwao, akiwa ni mwema basi husema: “Nitangulizeni [nitangulizeni] na akiwa si mwema basi husema: “Ee ole wangu! Wanalipeleka wapi?” Kila kitu husikia sauti yake isipokuwa mwanadamu. Lau angeisikia  basi ange[li]zimia.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/142), an-Nasaa´iy (01/270), al-Bayhaqiy na Ahmad (03/41, 58) kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Ziada mbili ni za an-Nasaa´iy, al-Bayhaqiy katika hizo mbili ni hiyo ya kwanza na Ahmad hiyo nyingine.

Ziada ya kwanza inatolewa ushuhuda na Hadiyth ya Abu Hurayrah ambaye amesema wakati alipofikiliwa na kifo:

“Msinizibe juu na wala msinisindikize kwa chetezo na mniwahishe. Kwani hakika mimi nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Anapowekwa mtu mwema juu ya kitanda chake cha jeneza basi husema: “Nitangulizeni…. “ mfano wa Hadiyth iliotangulia pasi na kutajwa: “Kila kitu husikia sauti yake.. “

Ameipokea an-Nasaa´iy na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (764), al-Bayhaqiy na at-Twayaalisiy (nambari. 2336), Ahmad (02/292, 274, 500) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za Muslim.

Ya tatu: ´Abdur-Rahmaan bin Jawshan ameeleza:

“Tulikuwa katika jeneza la ´Abdur-Rahmaan bin Samurah ambapo Ziyaad na watu katika watumwa wake wanatembea kwa miguu yao nyuma ya jeneza kisha wanasema: “Taratibuni, taratibuni Allaah akubarikini. Abu Bakrah akakutana nao katika baadhi vichochoro vya al-Madiynah akawakimbilia kwa nyumbu akiwaashiria bakora akisema: “Acheni! Naapa kwa Ambaye ameukirimu uso wa Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakika tumejikuta zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tunakaribia kutembea nalo matiti.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/65), an-Nasaa´iy (01/271), at-Twahaawiy (01/276), al-Haakim (01/255), al-Bayhaqiy (04/22), at-Twayaalisiy (883), Ahmad (05/36-38). al-Haakim amesema: “Swahiyh.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye na kabla yake an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/272). Ndani yake mna (05/271):

“Wanachuoni wamekubaliana juu ya kwamba imependekezwa kufanya haraka kumwandaa maiti. Isipokuwa kutapokhofiwa kutokana na kwenda haraka kupasuka kwa maiti, kubadilika kwake na mfano wa hayo. Katika hali hiyo watatembelea taratibu.”

Udhahiri wa amri unapelekea katika ulazima. Hayo pia ndio maoni ya Ibn Hazm (05/154-155). Hatukupata dalili itakayoigeuza kuipeleka katika mapendekezo. Hivyo tukasimamia hapo. Ibn-ul-Qayyim amesema katika “Zaad-ul-Ma´aad”:

“Ama kule kutembea kwa watu kwa upole hii leo hatua baada ya hatua ni Bid´ah yenye kuchukiza inayokwenda kinyume na Sunnah. Isitoshe ndani yake kuna kujifananisha na mayahudi na wakristo.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 08/07/2020