50. Baadhi ya fadhila za ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh)


Amesema mwandishi:

15- Sema “Watu bora baada ya Muhammad

    ni mawaziri wake, kisha ´Uthmaan [ndio maoni] yenye nguvu

MAELEZO

Watatu inapokuja katika ubora ni ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Yeye ni miongoni mwa wa awali waliotangulia katika Uislamu. Alihajiri mara mbili; alihajiri kwenda Habeshi na akahajiri kwenda al-Madiynah. Akajitolea mali tele katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall) na akanunua kisima cha warumi kwa ajili ya waislamu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni nani atayenunua kisima hichi na yuko na Pepo.”[1]

Akakinunua ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) na akakifanya ni Waqf kwa waislamu. Akaandaa jeshi la ´Usrah kikamilifu kutokana na mali yake. Yeye ndiye ambaye alishika uongozi baada ya ´Umar kwa maafikiano ya watu wa mashauriano ambao aliwateulia ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Wakampa kiapo cha usikivu na utiifu na waislamu kadhalika wakafanya hivo.

Isitoshe yeye ni mume wa wasichana wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni Ruqayyah na Umm Kulthuum. Ndio manaa akaitwa Dhun-Nurayn (aliye na nuru mbili) kwa kuwa alioa wasichana wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Makkah kuzungumza na washirikina na kukaenezwa uvumi kwamba ameuawa, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtolea bay´ah kwa mkono wake kwa kusema:

“Hii ni kwa ajili ya ´Uthmaan.”[2]

Bay´ah ikatimia pasi na yeye kuwepo kwa kuwa wakati huo alikuwa Makkah.

Kadhalika yeye ndiye ambaye aliandika msahafu unaoitwa “msahafu wa ´Uthmaan” kwa hati ya ´Uthmaan. Hati yake ndio hii misahafu tulionayo hii leo. Fadhila zake ni nyingi (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] al-Bukhaariy (2778)

[2] al-Bukhaariy (3698) na (4066)