Banuu Sa´d wakapata maombi kama wanaweza kumnyonyesha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tumepokea kwa mlolongo wa wapokezi ambao ni sahihi ya kwamba Haliymah as-Sa´diyyah ndiye ambaye alimnyonyesha. Akabaki kwake kwa Banuu Sa´d takriban miaka mine. Hapo ndipo kifua chake kikafunguka ambapo akamwagiza kwa mama yake. Mama yake akamchukua na kumsafirisha kwenda al-Madiynah kwenda kuwatembelea wajomba zake. Wakati alipokuwa anarudi Makkah akafa al-Abwaa´. Hapo alikuwa na miaka sita, miezi mitatu na siku kumi. Maoni mengine yanasema kuwa alikuwa na miaka mine.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake ya kwamba wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa njiani anaelekea Makkah mwaka wa Ufunguaji akapita al-Abwaa´. Akamuomba Mola Wake kutembelea kaburi la mama yake na akakubaliwa. Akalia na akawaliza wengine. Alikuwa pamoja naye wanaume elfu moja.

Wakati mama yake alipofariki Umm Ayman akamwangalia. Alikuwa ni kijakazi wake ambaye alimrithi kutoka kwa baba yake. Siku hizo aliishi chini ya uangalizi wa babu yake ´Abdul-Muttwalib. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofikisha miaka nane babu yake akafariki ambaye hapo kabla alikuwa ameacha amemuusia ami yake Abu Twaalib amwangalie. Abu Twaalib na baba yake ´Abdullaah walikuwa ni ndugu wa damu. Abu Twaalib akamwangalia vizuri kabisa. Alipokuwa Mtume akamnusuru kwa njia ya nguvu kabisa pamoja na kwamba aliendelea kubaki kwenye ushirikina wake mpaka alipofariki. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah akamkhafifishia adhabu yake, kama jinsi Hadiyth zilivyosihi juu ya hilo.

Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa na miaka kumi na mbili ami yake akamchukua na kwenda naye katika safari ya kibiashara kwa vile hakukuwepo na mtu mwingine wa kumwangalia Makkah. Wakati wa safari kuelekea Shaam yeye na wenzake wakaona ishara kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zilimfanya Abu Twaalib kuzidi kumwangalia. at-Tirmidhiy amepokea katika “al-Jaamiy´” yake kwa mlolongo wa wapokezi ambao wote ni waaminifu ya kwamba mawingu na miti vilimpa kivuli na mtawa Bahiyraa akatoa bishara njema juu yake na akamuamrisha ami yake kumrudisha ili mayahudi wasimwone wakaja kumdhuru. Hadiyth ina msingi ulio na asli na uko na nyongeza zingine.

Kisha akasafiri naye kwa mara nyingine kwenda Shaam kushughulikia biashara ya Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ´anhaa). Pamoja naye alikuwa na mtumwa wake wa kukopa Maysarah. Maysarah akaona hali ya kipaji chake na baadaye akamueleza bosi wake aliyoyaona. Khadiyjah akampendekeza amuoe kwa vile alikuwa akitarajia ile kheri ambayo Allaah amemtunukia yeye na zaidi ya hapo ambayo hakuna mtu anaweza kuifikiria. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuoa na huku yuko na miaka ishirini na tano.

Allaah (Subhaanah) alikuwa amemlinda tangu wakati alipokuwa bado ni mdogo. Alikuwa amemsafisha na sifa za machafu yote za kipindi kile cha kishirikina na aibu nyingine zote. Alikuwa amempamba kwa kila tabia nzuri mpaka akawa hajulikani kati ya watu wake isipokuwa kama “mwaminifu”. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakimwita baada ya kuona utwaharifu wake, ukweli wa maneno yake na uaminifu wake. Wakati alipokuwa na miaka thalathini na tano Quraysh wakaiboresha Ka´bah. Walipofikia kwenye jiwe jeusi wakaanza kugombana ni nani atakayeliweka jiwe mahala pake. Kila kabila linataka liweke. Hatimaye wakakubaliana wa kwanza atayewaingilia ndio ataliweka. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio akawa wa kwanza kuingia. Wakasema:

“Amekuja mwaminifu.”

Wakamkubalia. Akaamrisha kuletwe kitambaa. Akaliweka jiwe katikati ya kitambaa na akaamrisha kila kabila lishike kandoni mwa kitambaa kile. Halafu yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachukua jiwe la kuliweka mahala pake.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 18/03/2017