Mambo yenye kuvunja swawm ni manane:

La kwanza: Jimaa ikiwa na maana ya dhakari [tupu ya mwanaume] ikaingia kwenye utupu wa mwanamke wa mbele au wa nyuma. Pale tu mfungaji anapofanya jimaa swawm yake inavunjika. Ikiwa ni mchana wa Ramadhaan basi ni wajibu kwake vilevile kutoa kafara kubwa kutokana na ukubwa wa dhambi hiyo. Kafara inaanza kwa kuachia mtumwa huru. Ikiwa haiwezekani basi anatakiwa kufunga miezi miwili mfululizo. Ikiwa haiwezekani pia basi anatakiwa kulisha masikini sitini. Hukumu iko namna hii ikiwa ni wajibu kwake kufunga. Ikiwa swawm sio wajibu kwake – kama kwa mfano msafiri – anachotakiwa tu ni kulipa siku hiyo bila ya kutoa kafara.

 La pili: Kumwaga kwa kujitoa manii, kubusu, kukumbatia na mfano wa hayo. Hata hivyo hakumuwajibikii kitu ikiwa atambusu mke wake pasina kumwaga.

La tatu: Kula na kunywa. Swawm inavunjika chakula au kinywaji kikimezwa sawa ikiwa ni kupitia njia ya kinywa au pua. Haijalishi kitu ni aina gani ya chakula au kinywaji kinachomezwa. Haijuzu kwa mfungaji vilevile kuvuta moshi kwa njia ya kwamba ukaingia mwilini. Kwa sababu moshi una chembe ndogo ndogo. Hata hivyo ni sawa kunusa manukato.

La nne: Vitu vyenye maana ya kula na kunywa kama mfano wa sindano inayochukua nafasi ya chakula na kinywaji. Sindano nyinginezo hazivunji swawm sawa ikiwa sindano hiyo ni kupitia njia ya mishipa au mishipa ya damu.

La tano: Kuchota damu kama mfano wa kuumikwa [kupiga chuku], kuitoa kwa kukusudia na mengineyo mfano wa hayo yanayouathiri mwili kama jinsi kuumikwa kunavofanya. Hata hivyo kutoa damu kidogo, kama mfano wa damu ya kuangalia ugonjwa, ni kitu kisichovunja swawm kwa sababu ni jambo lisilouathiri mwili kama kuumikwa kunavofanya.

La sita: Kujitapikisha kwa makusudi.

La saba: Hedhi na nifasi.

Mambo haya yaliyotajwa hayavunji swawm isipokuwa kwa kutimia masharti matatu yafuatayo:

Ya kwanza: Mfungaji awe ni mwenye kujua hukumu na wakati.

Ya pili: Mfunga asiwe ni mwenye kusahau.

Ya tatu: Mfungaji afanye hivo kwa khiyari yake.

Hivyo lau mfungaji atapigwa chuku na huku afikiria kuwa chuku haivunji swawm, swawm yake ni sahihi kwa sababu ya ujinga wake wa kutokujua hukumu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini [itakuwa dhambi] katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu; na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (33:05)

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Mola Wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea.” (02:286)

Allaah akasema:

“Nimefanya hivo.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea jinsi ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) alivyoweka uzi myeusi na myeupe chini ya mto wake ambapo alikuwa akiziangalia [nyuzi hizo] wakati wa kula na kunywa. Wakati kulipokuwa kukibainika uzi mmoja kutokamana na mwingine ndipo anajizuia kula. Alikuwa anafikiria hiyo ndio maana ya Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Na kuleni na kunyweni mpaka ibainike kwenu weupe [wa afajiri] kutokana na weusi [wa usiku].” (02:187)

Alipomweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Huo ni weupe wa mchana na giza la usiku.”[1]

Pamoja na hivyo hakumwamrisha kurudi kufunga.

Mfano mwingine ni kama mtu atafikiria kuwa alfajiri haijaingia na kwamba jua limeshazama na akawa amekula kisha baadaye ikabainika kuwa alikosea. Huyu pia swawm yake ni sahihi kwa sababu hakujua wakati. al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Siku moja ambapo mawingu yalikuwa yametinga tulikata swawm katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya muda jua likachomoza.”[2]

Lau ingelikuwa ni wajibu kulipa basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelibainisha hilo. Kwa sababu Allaah ameikamilisha dini kupitia kwake. Na lau kama alibainisha hilo basi Maswahabah wangelitufikishia. Kwa sababu Allaah amejibebesha Mwenyewe jukumu la kuihifadhi dini. Pale tulipojua kuwa Maswahabah hawakufikisha hilo basi tukajua pia kuwa sio wajibu kwa sababu suala hili ni muhimu sana kiasi cha kwamba haliwezi kupuuzwa.

Hali kadhalika inahusiana na yule mtu aliyesahau kama amefunga na akaanza kula. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusahau pindi amefunga na akala au akanywa, akamilishe swawm yake. Allaah ndiye amempa chakula na kinywaji.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile swawm bado ni sahihi ikiwa mfungaji amelazimishwa kula, akameza maji kwa bahati mbaya wakati alipokuwa anasukutua mdomo, alipotumia dawa za matone ya maji kwenye macho na kwa bahati mbaya yakawa yameteremka mpaka tumboni na akaota wakati wa kulala. Kwa sababu hakuna lolote katika haya lililopitika kwa khiyari.

Siwaak haivunji swawm. Ni Sunnah kwa mfungaji na wengine kila nyakati kutumia Siwaak mchana mzima. Inajuzu kwa mfungaji kupunguza ukali wa joto na kiu kwa kuoga na mambo mengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijimwagia maji kichwani mwake kwa sababu ya kiu ilihali amefunga[4]. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alivaa nguo za kuloa wakati alipokuwa amefunga[5]. Ni katika wepesi ambao Allaah anatutakia. Himdi zote ni za Allaah kwa neema na usahilishaji Wake.

[1] al-Bukhaariy (1916) na Muslim (1090).

[2] al-Bukhaariy (1959).

[3] al-Bukhaariy (1933) na Muslim (1155).

[4] Abu Daawuud (2365).

[5] Ameipokea al-Bukhaariy kwa mlolongo wa wapokezi uliyopungua.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 03/06/2017