Amesema (Hafidhwahu Allaah) katika dibaji ya kitabu “Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah – fiyh-il-Hikmah wal-´Aql”:

“Wakati ilipokuwa ni wajibu kubainisha na kufichukua wapinzani na hali ya makundi mbalimbali ambayo yana khatari juu ya Uislamu na yanaweza kumzuia yule anayetaka kuingia katika Uislamu, baadhi yayo hayana lolote kuhusiana na Uislamu, kama Alivyosema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ

“Hakika wale waliofarakisha dini yao na wakawa makundimakundi, huna lolote kuhusiana na wao.”[1]

na Uislamu unaita kuwa na Umoja katika haki, kama Alivyosema (Ta´ala):

أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Simamisheni Dini na wala msifarikiane humo.”[2]

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja na wala msifarikiane!”[3]

likaanza kundi la wanachuoni wenye ghera na ukaguzi kuzindua makosa ya makundi haya na kubainisha jinsi wanavyoenda kinyume na mfumo wa Mitume katika kulingania. Wamefanya hili ili waweze kurejea katika usawa. Hakika ya haki ni kitu kilichompotea muumini. Lengo lingine ilikuwa ni yule asiyejua hali zao asije kutumbukia katika upotevu wao. Miongoni mwa wanachuoni hao ambao wamechukua jukumu hili kubwa na wakitendea kazi maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini ni nasaha. Dini ni nasaha. Dini ni nasaha.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah, kwa nani?” Akasema: “Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, watawala wa Waislamu na watu waliobaki.”

ni muheshimiwa Shaykh na Dr. Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy katika kitabu chake “Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah – fiyh-il-Hikmah wal- ´Aql” ambacho kipo mikononi mwetu. Amebainisha – Allaah Amuwafikishe na Amjaze kheri – mfumo wa Mtume katika kulingania katika Uislamu kwa njia iliyokuja katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani yake ameelezea mifumo ya makundi mbalimbali ili kuweka wazi tofauti kati ya mfumo wa Mtume na mifumo ya makundi hayo mbalimbali yanayoenda kinyume na mfumo wa Mitume. Ameijadili mifumo hiyo mjadala wa kielimu na uadilifu na kutumia mifano na ushahidi inayokazia. Kitabu chake kimetimiza lengo na kinatosheleza kwa yule anayetaka haki – na himdi zote ni Zake Allaah. Kadhalika ni hoja dhidi ya mwenye kufanya ukaidi na jeuri. Tunamuomba Allaah Amlipe kwa kazi yake na Awanufaishe wengine kwacho na swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake.”

Amesema pia katika dibaji ya kitabu chake “Jamaa´ah Waahidah laa Jamaa´aat” ambapo amemraddi ´Abdur-Rahmaan ´Abdul-Khaaliq:

“Kipindi cha mwisho kumejitokeza makundi mengi yanayojinasibisha na Da´wah na yanaenda chini ya uongozi maalum kwao. Kila kundi linajifanyia mfumo wao wenyewe, jambo ambalo linazalisha mfarakano, tofauti na ugomvi unaotokea kati ya makundi. Hili ni jambo ambalo linapingwa na Dini na linakataliwa na Kitabu na Sunnah. Wakati baadhi ya wanachuoni wanakataza njia hizi za kigeni ambazo wametumbukia ndani yake, baadhi ya ndugu wanaenda kinyume na kuwatetea. Miongoni mwa watetezi hawa ni muheshimiwa Shaykh ´Abdur-Rahmaan ´Abdul-Khaaliq. Hili linaonekana katika vitabu vyake vinavyochapishwa na kanda zinazosikilizwa pamoja na kwamba ndugu yake ameshamnasihi kuhusu hilo. Ukiongezea juu ya hilo akaanza pia kuwasema vibaya wanachuoni ambao hawakubaliani naye juu ya mambo yake. Akawasifu kwa maneno yasiyostahiki na hawakusalimika na hayo hata wale waalimu zake ambao walimsomesha. Muheshimiwa Shaykh Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy amesimama kidete na kumraddi katika kitabu hichi ambacho msomaji yuko nacho mbele yake kwa anwani “Jamaa´ah Waahidah laa Jamaa´aat wa Swiraatw Waahidah laa ´Asharaat”. Nimekisoma na nimekuta kuwa kimetimiza lengo na himdi zote ni Zake Allaah.”[4]

Aliulizwa pia swali tarehe tano Rabiy´ al-Awwal 1417 na akasema baada ya kumtaja Shaykh Rabiy´ na kundi katika wanachuoni:

“Miongoni mwa wanachuoni wanaojulikana ambao wana muda mrefu katika Da´wah, ni muheshimiwa Shaykh ´Abdul-Muhsin al-´Abbaad, muheshimiwa Shaykh Rabiy´ bin Haadiy, muheshimiwa Shaykh Swaalih as-Suhaymiy na muheshimiwa Shaykh Muhammad Amaan al-Jaamiy. Watu hawa wana juhudi na Ikhlaasw katika Da´wah. Wanawaraddi wale wanaotaka kwenda kinyume na Da´wah kutoka kwenye njia sahihi, pasi na kujali ikiwa atafanya hivo kwa kukusudia au kutokukusudia. Watu hawa wana uzowefu. Wana utafiti katika maoni mbalimbali na ufahamu wa kuyajua yaliyo ya sahihi na yasiyokua ya sahihi. Kwa ajili hiyo ni wajibu kusambaza kanda na duruus zao na mtu anufaike kwayo, kwa kuwa ndani yake kuna faida kubwa kwa Waislamu.”[5]

Vilevile amesema (Hafidhwahu Allaah) katika dibaji yake Radd ya Shaykh Rabiy´ kwa Hasan bin Farhaan al-Maalikiy:

“Nimekuta kuwa Radd ya Shaykh Rabiy´ ni yenye kutosheleza katika maudhui yake, nzuri katika usulubu wake na yenye kuponda upinzani. Allaah Amjaze kheri iliokuwa nzuri na Amlipe kwa kazi Aliyoifanya kwa kuinusuru haki na kuiponda batili na watu wake.”

Shaykh aliulizwa swali lifuatalo kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makkah tarehe kumi na tatu Jumaadah ath-Thaaniy 1424:

“Je, una nasaha yoyote ya kuwapa vijana ambao wanawasema vibaya baadhi ya maimamu wa Da´wah ya Salafiyyah kama Shaykh Muhammad Amaan al-Jaamiy na Shaykh Rabiy´ al-Madkhaliy?”

Akajibu:

“Tuacheni na watu binafsi na kueneza uvumi. Wanachuoni hawa, Allaah Akitaka, kuna kheri kwao. Kuna baraka kwao juu ya Da´wah ya Salafiyyah na kuwafundisha watu. Ikiwa baadhi ya watu hawakuridhika nao, basi itambulike kuwa si watu wote waliokuwa radhi na Mtume. Kulikuwepo watu waliomkasirikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Masuala ya nafsi zetu na matamanio yetu hayazingatiwi. Tunawadhania vyema wanachuoni. Hatujui lolote juu yao isipokuwa kheri tu, Allaah Akitaka, na tunawaombea Tawfiyq.”

[1] 06:159

[2] 42:13

[3] 03:103

[4] Tazama dibaji ya kitabu cha Shaykh Rabiy´ ”an-Naswr al-´Aziyz”

[5] al-As-ilah as-Swiydiyyah.

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.rabee.net/ar/sharticles.php?cat=12&id=57
  • Imechapishwa: 02/12/2019