13- Abu Hurayrah na Muslim wamepokea kupitia kwa Qabiyswah bin Mukhaariq al-Hilaal ambaye amesema:

“Nilikopa pesa na kuzitoa ili kutengeneza mafungamano kati ya watu na halafu baadae nikamjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuomba pesa. Akanambia: “Subiri mpaka pale tutapopata swadaqah kisha utapata.” Halafu akanambia: “Ee Qabiyswah! Kuomba sio halali isipokuwa kwa mmoja katika watu watatu. Mmoja wao ni yule anayekopa pesa na kuzitoa ili kutengeneza mafungamano kati ya watu. Anaweza kuomba mpaka pale atapolipa [deni lake]. Kisha baada ya hapo akome. Mwingine ni yule mwenye kufikwa na haja na akapoteza pesa zake. Anaweza kuomba mpaka pale atapoweza kujisimamia mwenyewe. Kisha baada ya hapo akome. Mwingine ni yule ambaye amefikwa na ufukara mpaka watu watatu katika watu wake wakasema kuwa amefikwa [kweli] na ufukara. Anaweza kuomba mpaka pale atapoweza kujisimamia mwenyewe. Ee Qabiyswah! Maombi mengine yote ni pesa ya haramu. Yule mwenye kuila anakula pesa ya haramu.”[1]

14- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema:

Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipothibitisha kanuni yenye kukataza kuomba na wakati huo huo watu wanaweza kufikwa na haja na ufukara na wakawa hawana budi kuomba, ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akabainisha wale wenye kutoka nje ya kanuni hii ya jumla na kusema:

“Kuomba sio halali isipokuwa kwa watu aina tatu tu.”

15- Kumepokelewa ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haifai kwa tajiri yeyote kupokea swadaqah isipokuwa watu tano: Mwenye kupigana katika njia ya Allaah, wal aamiliana alayha, ghaarimin, mwenye kuinunua kwa pesa zake na mtu ambaye ana jirani ambaye ni masikini akampa nayo na [baada ya kumpa] masikini huyo akamzawadia nayo.”[2]

Hadiyth inatolea dalili na kuonesha kuwa kuna hali yenye kumjuzishia tajiri kupokea zakaah na kuomba. Inafasiri maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Si halali kumpa swadaqah tajiri na yule ambaye ana nguvu.”

Maneno yake [yaliyoko] juu yako kwa jumla na yanakhusishwa na Hadiyth ya watu watano na Hadiyth ya Qabiyswah.

16- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna watu ambao ni funguo za kheri na wanafunga mambo ya shari na kuna watu ambao ni funguo za shari na wanafunga mambo ya kheri. Pepo iwe kwa yule ambaye Allaah amefanya funguo za kheri kupitia mikononi mwake na ole wale yule ambaye Allaah amefanya funguo za shari kupitia mikononi mwake.”[3]

[1] Muslim (1044).

[2] Ahmad (3/56), Abu Daawuud (1636) Ibn Maajah (1841) na al-Haakim (1/407) ambaye amesema kuwa Hadiyth iko kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

[3] Ibn Maajah (237), at-Twayaalisiy (208) na Ibn Abiy ´Aaswim katika ”as-Sunnah” (299). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhilaal-ul-Jannah” (297-299).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 21-25
  • Imechapishwa: 18/03/2017