Ndugu! Mimi nitakuulizeni kwa jina la Allaah na nitakuombeni mnijibu kwa akili zenu timamu na sio kwa hisia zenu, kwa mujibu wa inavosema dini yenu na sio kwa kufuata kichwa mchunga. Mnasemaje juu ya wale wenye kuzua ndani ya dini ya Allaah – pasi na kujali ikiwa Bid´ah hizo zinahusiana na dhati ya Allaah, sifa na majina Yake au ikiwa inahusiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na kusema kuwa wao eti ndio wanamuadhimisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); je hawa wanamuadhimisha Allaah na Mtume Wake bora kuliko wale wasioenda kinyume na Shari´ah ya Allaah kwa kiasi cha milimita moja, wakaiamini na wakaisadikisha, wakajisalimisha na maamrisho na makatazo, hawatangulii mbele ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mbele ya chochote kisichokuwemo katika dini ya Allaah? Bila ya shaka hawa wa pili ndio wenye kumuadhimisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wenye kuonyesha kuwa kweli wanampenda Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawazui.

Ni jambo lenye kushangaza kwelikweli kuona watu hawa wanayajua maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”[1]

na kwamba inakusanya na kunaingia ndani yake Bid´ah sampuli zote. Alikuwa ni kiumbe mfaswaha zaidi na mwenye kuwatakia mema viumbe zaidi. Hatamki kitu isipokuwa kitu alichokusudia maana yake. Kwa hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anajua anachokisema pale aliposema:

“… na kila Bid´ah ni upotevu…”

Alikuwa anajua maana ya anachokisema. Alisema hivyo kwa sababu anautakia Ummah wake mema. Kwenye maneno yake kumetimia mambo matatu:

1 – Ukamilifu wa kuwatakia watu mema.

2 – Ukamilifu wa bayana na ufaswaha.

3 – Ukamilifu wa elimu na hekima.

Pasi na shaka yoyote ni dalili yenye kuonyesha kuwa maneno yake yanatakiwa kufahamika kama yalivyo. Hivyo basi, ni jambo la kuwezekana kuzigawa Bid´ah katika mafungu matatu au matano? Si sahihi kabisa.

[1] Ahmad (17275), Abu Daawuud (4607), Ibn Maajah (42) na at-Tirmidhiy (2676) ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh na al-Haakim ameisahihisha (01/95) na adh-Dhahabiy ameafikiana naye na wao wameipokea pasi na:

”… na kila upotevu ni Motoni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 6-8
  • Imechapishwa: 23/10/2016