49. Wanawake kulisindikiza jeneza na usindikizaji wa sauti kwa kelele

46- Fadhilah hizi za kulisindikiza jeneza ni kwa wanaume peke yao pasi na wanawake. Hilo ni kutokana na makatazo yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yao kuliandama. Ni makatazo ya kujikatasa. Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Tulikuwa tukikatazwa [katika upokezi mwingine imekuja: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza] kulisindikiza jeneza na wala hakututilia mkazo.”

Ameipokea al-Bukhaariy (01/328-329, 03/162), Muslim (03/47) na mtiririko ni wake, Abu Daawuud (02/63), Ibn Maajah (01/487), Ahmad (06/408, 409) na kadhalika al-Bayhaqiy (4/77), al-Ismaa´iliy upokezi mwingine ni wake na ni upokezi wa al-Bukhaariy hali ya kuiwekea taaliki.

47- Haijuzu kulisindikiza jeneza kutokana na yale yanayokwenda kinyume na Shari´ah. Maandiko yamepokelewa juu ya hayo kwa mambo mawili: kupaza sauti kwa kilio na kulisindikiza kwa moshi. Hayo ni katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msilifuati jeneza kwa sauti wala moto.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/64), Ahmad (02/427, 528, 532) kupitia kwa Abu Hurayrah.

Katika cheni ya wapokezi wake yuko ambaye hakutajwa jina. Lakini inapata nguvu kwa shawahidi zake zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baadhi ya mapokezi yaliyoishilia kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Kuhusu shawahidi imepokelewa kutoka kwa Jaabir ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kumsidikiza maiti kwa sauti wala moto. al-Haythamiy (03/29) amesema:

“Ameipokea Abu Ya´laa na humo yuko ambaye hakutajwa.”

Iko katika “al-Musnad Abiy Ya´laa” (2627) na humo yumo ´Abdullaah bin al-Muharram ambaye Hadiyth zake ni munkari. Kinachodhihiri ni kwamba bwana huyu ameharirika kwa al-Haythamiy na ndio maana hakumjua.

Ibn ´Umar amepokea akisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulifuata jeneza sambamba na sauti ya fujo.”

Ameipokea Ibn Maajah (01/419-480), Ahmad (5668) kupitia njia mbili kutoka kwa Mujaahid kutoka kwake. Ni Hadiyth nzuri kwa mkusanyiko wa njia zake mbili.

Kutoka kwa Abu Muusa kuhusu makatazo ya kumsindikiza maiti kwa chetezo. Matamshi yake yamekwishatangulia katika masuala ya 21 nambari. 02 ukurasa wa 08.

Ama kuhusu mapokezi kutoka kwa ´Amr bin al-´Aasw kwamba alisema katika wasia wake:

“Mimi nitapokufa basi asinisindikize mwombolezaji wala moto.”

Ameipokea Muslim (01/78) na Ahmad (04/199).

Kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba alisema wakati alipofikiliwa na maiti:

“Msinizibe juu na wala msinisindikize kwa chetezo [katika upokezi mwingine imekuja: “Kwa moto.”]

Ameipokea Ahmad na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kama itavokuja baada ya masuala haya.

48- Kunaingia katika hayo [ya kutokujuzu] kunyanyua sauti kwa Dhikr mbele ya jeneza. Kwa sababu kitendo hicho ni Bid´ah. Pia kutokana na maneno ya Qays bin ´Abaad:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakichukia kunyanyua sauti wakati wa kusindikiza jeneza.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/74), Ibn-ul-Mubaarak katika “az-Zuhd” (83) na Abu Nu´aym (09/85) kwa cheni ya wapokezi ambao ni wenye kuaminiwa.

Jengine ni kwa sababu sisi kufanya hivo ni kujifananisha na wakristo kwa sababu wao wananyanyua sauti zao kwa kusoma sehemu katika injili yao na nyiradi zao pamoja na kurefusha maneno, kuimba na sauti za huzunihuzuni.

Baya zaidi kuliko yote hayo ni kuyasindikiza kwa kupiga muziki kwa kutumia ala za muziki mbele yake muziki wenye huzunihuzuni, kama inavofanywa katika baadhi ya miji ya Kiislamu kwa ajili ya kuwaigiliza makafiri. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.

an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Adhkaar”, uk. 203:

“Tambua kwamba maoni ya sawa, yenye kuchaguliwa na matendo ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) ni kunyamaza wakati wa kulisindikiza jeneza. Kwa hiyo haifai kunyanyua sauti kwa kisomo, Dhikr wala kitu kingine.

Hekima ya hilo iko wazi. Nayo ni kwamba hilo linatuliza zaidi moyo wake na kuziweka mahala pamoja fikira zake juu ya yale yanayohusiana na jeneza, jambo ambalo linatakikana katika hali hii. Hii ndio haki. Usidanganyike na wengi wanaokwenda kinyume na jambo hili. Abu Ya´laa al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Radhiya Allaahu ´anh) amesema maneno yenye maana kama ifuatayo:

“Lazimiana na njia ya uongofu na wala usidanganyike na uchache wa wenye kuifuata na jihadhari na njia za upotevu na usidanganyike na wengi wa wenye kuifuata.”

Tumepokelewa katika “Sunan al-Bayhaqiy” yanayopelekea katika yale niliyoyasema mimi (anaashiria maneno ya Qays bin ´Ubaad). Kuhusu yale yanayofanywa na wajinga kuyasomea majeneza huko Dameski na kwenginepo katika kusoma kwa kurefusha na kuyaondosha maneno kutoka mahala pake stahiki ni jambo la haramu kwa maafikiano ya wanachuoni. Nimeyaweka wazi ubaya wake, ukali wa uharamu wake na dhambi nzito za yule aliyeweza kuyakemea lakini akaacha kufanya hivo katika katika “Aadaab-ul-Qiraa-ah”. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.”

Anaashiria kitabu chake “at-Tibyaan fiy Aadaab Hamalat-il-Qur-aan”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 90-93
  • Imechapishwa: 06/07/2020