49. Uwajibu wa mwanamke kumhudumia mume wake

Baadhi ya Hadiyth zilizotajwa punde tu ni dalili za wazi kabisa juu ya uwajibu wa mwanamke kumtii mume wake na kumhudumia katika mpaka wa uwezo wake. Miongoni mwa mambo yasiyokuwa na shaka jambo la kwanza linaloingia katika hayo ni kuhudumu katika nyumba yake na yale mengine yanayohusiana na hilo kama vile kuwalea watoto na mfano wake. Wanachuoni wametofautiana juu ya hili. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Wanachuoni wametofautiana kama ni wajibu kwa mke kumhudumia katika fenicha za nyumba, kuandaa chakula, vinywaji, kusaga unga, kupika chakula kwa ajili ya watumwa wake na kuwalisha farasi na mfano wa hayo. Wapo waliosema kuwa si wajibu kuyafanya hayo. Maoni haya ni dhaifu. Ni kama maoni yanayosema kwamba si wajibu kwa mume kutangamana na mke kwa uzuri na kumwingilia mkewe. Kwani huku sio kutangamana na mume kwa uzuri. Mke ni kama rafiki nyumbani – kama  alivyo rafiki wa mtu safarini – asipomsaidia katika yale mambo ya manufaa yake basi atakuwa si mwenye kutangamana naye kwa uzuri. Imesemekana vilevile – na ndio maoni ya sawa – ya kwamba ni wajibu kumhudumia. Mume ndiye bwana wake kwa mujibu wa Qur-aan na mke ndiye msaidizi wake kwa mujibu wa Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ilivyotangulia katika ukurasa wa 270. Kwa hivyo mtumwa na mateka wanapaswa kuhudumiwa na kwa sababu hivyo ndivyo kutaamiliana kwa wema.

Isitoshe wapo waliosema kwamba ni wajibu kumhudumia huduma nyepesi na ya kawaida. Wapo wengine waliosema kwamba ni wajibu kumhudumia huduma njema. Haya ndio maoni ya sawa. Ni wajibu kwake kumhudumia huduma njema na yenye kutambulika kama ya anayomfanyia. Hili linatofautiana kutegemea na hali. Huduma za mwanamke wa shambani si kama huduma za mwanamke wa kijijini na huduma za mwanamke mwenye nguvu si kama huduma za mwanamke ambaye ni dhaifu.”[1]

 Hii ndio haki – Allaah (Ta´ala) akitaka – ya kwamba ni wajibu kwa mwanamke kuhudumia nyumbani. Hayo ndio maoni ya Maalik na Aswbagh kama ilivyo katika “al-Fath” (09/418), Abu Bakr bin Abiy Shaybah, pia al-Jawzjaaniy kutoka katika Hanaabilah kama ilivyo katika “al-Ikhtiyaar”, uk. 145 na kundi katika Salaf na waliokuja nyuma vilevile kama ilivyo katika “az-Zaad” (04/46). Wale waliosema kuwa sio wajibu hatujaona dalili yoyote ya sawa. Maneno ya baadhi yao wanaosema kwamba:

“Ufungaji wa ndoa kunapelekea katika kustarehe kijimai na sio kuhudumika”

ni yenye kutupiliwa mbali. Kwa sababu mwanamke pia anapata kustarehe kijimai kutoka kwa mume wake. Wawili hao ni wenye kushirikiana inapokuja katika suala hilo.

Kama inavyotambulika Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amemuwajibishia mume mume jambo jengine. Nalo si jengine isipokuwa ni kumpa matumizi, mavazi na makazi. Kwa hiyo uadilifu unapelekea kuwa ni wajibu kwa mke kuyakabili hayo kwa kitu kingine. Nacho si kingine isipokuwa ni kumhudumia mumewe na khaswa ukizingatia ya kwamba yeye ndiye msimamizi wake kwa mujibu wa dalili ya Qur-aa tukufu, kama ilivyotangulia. Mwanamke asiposimama kumhudumia basi mume ndiye atalazimika kumhudumia nyumbani, jambo ambalo litapelekea yeye mwanamke ndiye awe msimamizi wake – jambo ambalo linaenda kinyume na Aayah ya Qur-aan kama isivyofichika. Hivyo basi imethibiti ya kwamba ni lazima kwake mwanamke kumhudumia mumewe. Haya ndio malengo.

Vilevile mume kumhudumia mke kutapelekea katika mambo mawili yenye kugongana kabisa kwamba mume atashughulika na kuzuilika kutokamana na kutafuta riziki na manufaa mengine na huku mwanamke atabaki nyumbaki akiwa hana kazi yoyote ambayo ni wajibu kwake kuifanya. Haufichiki ufisadi wa jambo hili katika dini ambayo imefanya sawa kati ya mume na mke inapokuja katika haki mbalimbali. Sivyo tu bali imemfadhilisha mwanaume juu yake kwa daraja nyingi. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusikiliza malalamiko ya msichana wake Faatwimah pindipo:

“Alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumshtakia ugumu wa kazi za mikononi anazokutana nazo nyumbani pamoja na kuwa hakumkuta baba yake ambapo akamwachia ujumbe ´Aaishah. Alipokuja (´alayhis-Salaam) ´Aaishah akamweleza. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) anaelezea: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatujia na akakuta tayari tumeshapanda juu ya kitanda ambapo tukataka kusimama akasema: “Hapo hapo mlipo! Je, nisikuelezeni katika jambo bora kuliko kile mlichokiomba? Mnapopanda kitandani kwenu basi semeni “Subhaan Allaah” mara thelathini na tatu, “Alhdmulillaah” mara thelathini na tatu, “Allaahu Akbar” mara thelathini na nne, hivo ni bora kwenu kuliko mtumishi.” ´Aliy anasema: “Hatukupatapo kuacha kufanya hivo.” Akaulizwa: “Hata katika usiku wa Swiffiyn?” Akasema: “Hata katika usiku wa Swiffiyn.”

Ameipokea al-Bukhaariy (09/417-418)

Kwa hiyo wewe mwenyewe unaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumwambia ´Aliy kwamba si lazima kwa Faatwimah kumhudumia. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si mwenye kupendelea hukumu kwa yeyote, kama alivyosema Ibn-ul-Qayyim (Radhiya Allaahu ´anh). Anayetaka kutafiti zaidi juu ya masuala haya basi arejee katika kitabu chake chenye thamani “Zaad-ul-Ma´aad” (04/45-46).

Kuhusu yaliyotangulia kwamba ni lazima kwa mwanamke kumhudumia mumewe hakuzuii yale mapendekezo ya mume kumsaidia katika hayo pindi atapopata nafasi na wakati. Bali kufanya hivo ni katika kutangamana kwa wema baina ya mume na mke. Kwa ajili hiyo ndio maana mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa kuwahudumia familia yake. Pindi wakati wa swalah unapotika anatoka na kwenda kuswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy (02/129) na (09/418), at-Tirmidhiy (03/314 ) ambaye ameisahihisha. Nimeipokea katika “ash-Shamaa-il” (02/185) kupitia njia nyingine kutoka kwa ´Aaishah huyohuyo kwa tamko:

“Alikuwa ni mtu kama watu wengine; akishughulikia nguo zake na akijihudumia mwenyewe.”

Wapokezi wake ni wapokezi Swahiyh na katika baadhi yake kuna udhaifu[2]. Lakini ameipokea Ahmad, Abu Bakr ash-Shaafi´iy kwa mlolongo wa wapokezi wenye nguvu kama nilivyohakikisha hayo katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (670).

Hapa ndipo mwisho ambapo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ametuwafikisha kuyakumbusha katika kitabu hichi kuhusu “Aadaab-uz-Safaaf”.

 

سبحانك اللهم وبحمدك أشهد أن لا إله إلا أنت أستغفرك وأتوب إليك

Kutakasika kutokamana na mapungufu ni Kwako, ee Allaah, himdi zote ni Zako na nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe, nakuomba msamaha na kutubia Kwako.

[1] al-Fataawaa (02/234-235)

[2] Kwa ajili hiyo ndio maana mfanyaji wa taaliki wa “Sharh-us-Sunnah” (13/243/3676) ameidhoofisha na mimi nikapitwa na njia yenye nguvu ambayo nitaiashiria punde kidogo. Ukitaka rejea katika kitabu changu “Mukhtaswar-ush-Shamaa-il” (293).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 286-291
  • Imechapishwa: 20/05/2018