49. Nyakati ambazo du´aa ina matumaini makubwa ya kuitikiwa

Swali 49: Je, wakati ambao du´aa inaitikiwa ni ile saa ya mwisho wakati wa alasiri? Je, ni lazima kwa muisamu kuwepo ndani ya msikiti katika saa hii na vivyo hivyo wanawake[1]?

Jibu: Kuna maoni mawili yenye nguvu zaidi juu ya saa ambayo du´aa ni yenye kuitikiwa:

1 – Baada ya ´Aswr mpaka kuzama kwa jua kwa ambaye ameketi na anasubiri swalah ya Maghrib. Ni mamoja atakuwepo msikitini au nyumbani kwake akimwomba Mola Wake. Ni mamoja ni mwanamme au mwanamke. Katika hali hii yuko karibu zaidi na kuitikiwa. Lakini haifai kwa mwanamme kuswali nyumbani swalah ya Maghrib wala nyengine isipokuwa kwa dalili ya ki-Shari´ah kama inavotambulika kutokana na dalili za ki-Shari´ah.

2 – Ni tokea pale ambapo imamu anapoketi juu ya mimbari kwa ajili ya kutoa Khutbah siku ya ijumaa mpaka kumalizika kwa swalah. Du´aa katika nyakati hizi mbili iko karibu zaidi na kujibiwa.

Nyakati mbili hizi ndio ziko karibu zaidi na kuitikiwa siku ya ijumaa. Kumepokelewa juu yake Hadiyth Swahiyh zinazofahamisha juu ya hilo. Nyakati hizi zinatarajiwa vilevile katika masaa ya masiku mengine. Fadhilah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni pana.

Miongoni mwa nyakati za kujibiwa saa ni katika swalah nyenginezo ambazo ni za faradhi na zilizopendekezwa katika hali ambapo mtu amesujudu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mja anakuwa karibu zaidi na Mola Wake ambapo amesujudu. Hivyo ombeni du´aa kwa wingi.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

Muslim (Rahimahu Allaah) amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ama katika Rukuu´ muadhimisheni na ama katika Sujuud jitahidini katika du´aa. Kuna matumaini makubwa na nyinyi kuitikiwa.”[3]

Maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna matumaini makubwa na nyinyi kuitikiwa.”

Bi maana ni karibu zaidi.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/402-404).

[2] Ahmad (9165) na Muslim (482).

[3] Ahmad (1903) na Muslim (479).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 100-101
  • Imechapishwa: 05/12/2021