49. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Tunapomuonjesha rehema kutoka Kwetu baada ya dhara iliyomgusa, bila shaka husema: “Haya nayastahiki mimi na sidhani kama Saa itatokea.”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ رَحْمَةً مِّنَّا مِن بَعْدِ ضَرَّاء مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ هَذَا لِي وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً

”Tunapomuonjesha rehema kutoka Kwetu baada ya dhara iliyomgusa, bila shaka husema: “Haya nayastahiki mimi na sidhani kama Saa itatokea.” (Fuswswilat 41:50)

Mujaahid amesema:

“Hili ni kutokana na matendo yangu na mimi ndiye mwenye kuiistahiki.”

Ibn ´Abbaas amesema:

“Bi maana kilichokuwa kwangu.”

2-

قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَى عِلْمٍ عِندِي

“Akasema: “Hakika [ninayomiliki] nimepewa haya kwa sababu ya elimu yangu.” (al-Qaswasw 28:78)

Qataadah amesema:

“Bi maana kutokana na elimu yangu kwa sababu ya uzoefu wa njia mbalimbali za kuchuma.”

Wengine wakasema:

“Ni kutokana na elimu ya Allaah kwa sababu mimi ndiye mwenye kuistahiki.”

Hii ndio maana ya maneno ya Mujaahid:

“Nimeipewa kwa sababu ya utukufu wangu.”

3- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kuna watu watatu katika wana wa israaiyl, mwenye ukoma, kipara na kipofu. Allaah akataka kuwajaribu ambapo akawatumia Malaika. Malaika yule akamwendea yule aliyekuwa na ukoma na akamwambia: “Kitu gani unachokipenda sana?” Akajibu: “Rangi nzuri na ngozi nzuri na niondokwe na haya ambayo watu huniona ni mchafu kwayo.” Malaika yule akampapasa na uchafu wake ukaondoka na pia akapewa rangi nzuri na ngozi nzuri. Akamuuliza tena: “Mali ipi unayopenda sana?” Akajibu: “Ngamia (au ng´ombe, Ishaaq ametilia shaka).” Akapewa ngamia kumi. Kisha Akamwambia: “Allaah akubarikie ngamia hawa.” Akamwendea yule wa kipara na kumuuliza: “Ni kitu gani unachokipenda sana?” Akajibu: “Kupata nywele nzuri na yaniondoke haya ambayo watu huniona mchafu kwayo.” Malaika akampapasa ambapo akaondokwa na uchafu wake na akapewa nywele nzuri. Akamuuliza tena: “Mali ipi unayopenda sana?” Akajibu: “Ng´ombe au ngamia.” Akapewa ng´ombe mwenye mimba na kumwambia: “Allaah akubarikie ng´ombe wako hawa.” Akamwendea kipofu na kumuuliza: “Ni kitu gani unachokipenda sana?” Akasema: “Allaah anirudishie macho yangu niweze kuwaona watu.” Akampapasa ambapo Allaah akamrudishia macho yake. Kisha akamuuliza tena: “Ni mali ipi unayopenda sana?” Akajibu: “Kondoo.” Akapewa kondoo wenye mimba. Baadaye wale wanyama wote watatu wakashika mimba na kuzaana, huyu akawa na zizi la ngamia, huyu akawa na zizi la ng´ombe na huyu akawa na zizi la kondoo.” Halafu Malaika yule akamwendea yule wa ukoma akiwa katika hali na umbo lake lilelile la mara ya kwanza na akamwambia: “Mimi ni mtu masikini na nimekatikiwa na nyenzo zangu katika safari yangu. Sina cha kunifikisha leo isipokuwa kwa msaada wa Allaah kisha msaada wako. Ninakuomba kwa Jina la yule Aliyekupa rangi nzuri, ngozi nzuri na mali unipe ngamia mmoja atakayenifikisha katika safari yangu.” Akajibu: “Nina majukumu mengi.” Malaika yule akamwambia: “Kana kwamba mimi nakujua, kwani wewe hukuwa na ukoma watu wanakuona mchafu tena fakiri kisha Allaah ndio akakupa mali?” Akajibu: “Mimi nimeirithi mali hii kutoka kwa mababu zangu.” Malaika yule akasema: “Ikiwa umesema uongo, basi Allaah akurudishe katika hali uliokuwa nayo mwanzo!” Malaika yule akamwendea mtu wa kipara kwa hali yake na umbo lilelile na akamwambia kama alivyomwambia huyu wa kwanza ambapo akamjibu kama alivyomjibu yule wa kwanza. Akamwambia: “Ikiwa umesema uongo, basi Allaah akurudishe katika hali uliokuwa nayo mwanzo!” Akamwendea yule kipofu kwa hali yake na uombo lilelie na kumwambia: “Mimi ni mtu masikini na msafiri; nimekatikiwa na nyenzo zangu katika safari yangu. Sina cha kunifikisha leo isipokuwa kwa msaada wa Allaah kisha msaada wako. Ninakuomba kwa Jina la yule Aliyekurudishia macho yako unipe kondoo mmoja atakayenifikisha katika safari yangu.” Akajibu: “Kwanza mimi nilikuwa kipofu ambapo Allaah akanirudishia macho yangu. Chukua unachokitaka na uache unachokitaka. Ninaapa kwa Allaah kwamba sintokuzuia kuchukua chochote unachokichukua kwa ajili ya Allaah.” Malaika yule akamwambia: “Baki na mali yako. Hakika mmepewa majaribio na Allaah amekuridhia wewe na amewakasirikia wenzako wawili.”[1]

MAELEZO

Mwandishi ameandika mlango huu ili kuonyesha namna watu wengi wanavyokanusha neema na kutokukubali kwamba wametunukiwa nazo na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ رَحْمَةً مِّنَّا مِن بَعْدِ ضَرَّاء مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ هَذَا لِي وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً

”Tunapomuonjesha rehema kutoka Kwetu baada ya dhara iliyomgusa, bila shaka husema: “Haya nayastahiki mimi na sidhani kama Saa itatokea.”

Aayah inaonyesha haya ndio maumbile ya mwanadamu isipokuwa wale waliokingwa na Allaah. Anakanusha neema na kutokukubali kuwa zinatoka kwa Muumba wao (´Azza wa Jall). Namna hii ndivyo alivyo mwanadamu anakanusha neema na kusema kwamba inatokamana na matendo yake mwenyewe, bidii zake na kadhalika.

Malengo ya mlango huu ni kumuhimiza mwanadamu juu ya kumshukuru Allaah kwa neema na kuzinasibisha Kwake. Hata kama mwanadamu ndiye katenda lakini hata hivyo ni kutokana na fadhilah za Allaah. Yeye ndiye kamfanyia mimea kukuwa. Yeye ndiye kamfanyia wepesi biashara na kumfanya akaweza kufaidika. Hakuna neno akaelezea sababu zilizopelekea kumfikisha huko, lakini kwanza anatakiwa kubainisha kwamba neema hizo zinatokamana na Allaah na kumshukuru. Lakini kilichokatazwa ni kuziegemeza katika sababu na kumsahau Yule mneemeshaji.

3- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kuna watu watatu katika wana wa israaiyl, mwenye ukoma, kipara na kipofu… “

Katika Hadiyth hii kuna faida kubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametusimulia nacho kutokana na mazingatio yake na ili tusitumbukie katika yale waliyotumbukia wana wa israaiyl.

Watu hawa watatu Allaah aliwajaribu kwanza kwa kuwapa madhara ya wakati mgumu kisha kwa kuwapa wakati wa raha. Wale wawili wakazikufuru neema za Allaah na yule mmoja akazishukuru. Haya yanatilia nguvu maneno Yake Allaah:

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

“Wachache miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru.” (Sabaa´ 34:13)

[1] al-Bukhaariy (3464) na Muslim (2964).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 146-147
  • Imechapishwa: 05/11/2018