49. Mfumo wa kikomunisti dhidi ya Ahl-us-Sunnah


Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtapata viongozi ambapo kuna vitu mtavitambua na vyengine hamtovitambua. Yule atakayekemea basi amesalimika na yule mwenye kuchukia ametakasika. Tatizo liko kwa yule atakayeridhia na kufuata.” Wakasema: “Ee  Mtume wa Allaah! Tusiwapige vita?” Akasema: “Hapana, maadamu wanaswali.”[1]

Muslim amesema:

“Bi manaa yule mwenye kuchukia na kukemea kwa moyo wake.”

Muslim anachomaanisha ni kwamba mtu anaweza kuchukia na kukemea kwa moyo kwa wakati mmoja. Hadiyth nyingine inasema:

“Yule katika nyinyi atakayeona mauvo basi ayakemee kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ndio imani dhaifu kabisa.”[2]

Leo ikiwa mwanachuoni hawezi kukemea isipokuwa kwa moyo wake peke yake ima kwa sababu ya kuogopa au kwa sababu nyingine, anatuhumiwa kuwa ni kibaraka, jasusi, mpakanaji mafuta na tuhuma nyenginezo ambazo hawakuzitoa kwenginepo isipokuwa kutoka kwa wakomunisti. Hizi sio nyenendo zinazotoka kwa waislamu. Hii ni mienendo ya wakomunisti, wafanya mapinduzi, wafuasi wa kundi la Ba´th, wazalendo na makundi mengine potofu. Ni vipi kijana wa Kiislamu anaweza kukubali kitu kama hicho? Wanachuoni wa Uislamu na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kushikamana barabara na maelekezo ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama mfano wa haya, maoni ya maimamu, akiwemo Maalik, ash-Shaafi´iy, Ahmad bin Hanbal, al-Awzaa´iy, ath-Thawriy na wengineo. Wote hawa waliishi chini ya serikali zilizokuwa na makosa na upindaji. Kulipitika nini kipindi cha Imaam Ahmad? Nchi iliyokuwa ikipinga sifa za Allaah na ikiwa na fikira za Jahm. Fikira za Jahm zina kufuru. Nadharia inayosema kuwa Qur-aan imeumbwa ni kufuru kwa mujibu wa Ahmad na Ahl-ul-Hadiyth wengine katika wakati huo. Serikali ilikuwa ikiita katika kufuru. Pindi walipotaka kufanya uasi Imaam Ahmad akakataa na kusema kuwa kitendo hicho sio salama na kinawadhuru waislamu. Akawakemea. Je, Ahmad alikuwa mwoga? Je, Ahmad alikuwa kibaraka? Salaf ndio waliokuwa wakifuata dalili hizi.

Khawaarij na watu wa fitina wengine katika Mu´tazilah na wengineo wanatutuhumu sisi kuwa ni vibaraka na majasusi. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba wanawapiga vita Ahl-us-Sunnah kwa kutumia mifumo ya wakomunisti, kundi la Ba´th, wazalendo na makundi mengine ya ukanajimungu. Ni vipi wanaweza kuitumia mifumo hii kwa waislamu na kutochukua dalili hizi? Ni kwa nini wasiwape udhuru wale walio na dalili hizi? Tuseme kuwa kweli mimi sitaki kufanya uasi. Simkufurishi kiongozi. Wewe ndiye unafuata madhehebu ya Khawaarij na unamkufurisha. Achana na mimi usinitweze. Ni wajibu kwako kusikiliza maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hapana, maadamu wanasimamisha swalah.”

“Hapana, maadamu wanaswali.”

“Mpaka pale mtakapoona kufuru ya wazi ambayo mna dalili kwayo kutoka kwa Allaah.”

[1] Muslim (1854).

[2] Muslim (49).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 420-421
  • Imechapishwa: 07/11/2017