Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya shahaadah ni maneno Yake (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلا هُوَ وَالْمَلائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِماً بِالْقِسْطِ لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye na Malaika, na wenye elimu [wote wameshuhudia kwamba Yeye] ni Mwenye kusimamisha [uumbaji Wake] kwa uadilifu – hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.” (Aal ´Imraan 03 : 18)

MAELEZO

Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ni nguzo moja. Licha ya kuwa ni sentesi mbili pamoja na hivyo ni nguzo moja kwa kuwa ´ibaadah zimejengeka juu ya kuhakikisha hayo mawili kwa pamoja. ´Ibaadah haikubaliwi isipokuwa kwa kumtakasia dini Allaah (´Azza wa Jall), jambo ambalo limefungamana na kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo limefungamana pia na kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Katika Aayah tukufu Allaah anajitolea ushahidi Mwenyewe na ushahidi wa Malaika na ushahidi wa wanachuoni ya kuwa hakuna anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye na kwamba ni Mwenye kusimamisha kwa uadilifu. Halafu akathibitisha hayo kwa kusema:

لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.”

Katika Aayah hii kuna sifa na nafasi kubwa walionayo wanachuoni pindi aliposema kwamba wanachuoni wanashuhudia pamoja na Yeye na Malaika. Makusudio ya wanachuoni hapa ni wale walio na elimu juu ya Shari´ah na wanaochukua nafasi ya mbele kabisa ni Mitume watukufu.

Shahaadah hii ni shahaadah kubwa kutokana na ukubwa wa mwenye kushuhudia na mwenye kushuhudiwa. Wenye kushuhudia ni Allaah, Malaika Wake na wanachuoni, wakati mwenye kushuhudiwa ni kupwekeka kwa Allaah katika haki Yake ya kuabudiwa. Kitu ambacho kinathibitisha hilo ni:

لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 70
  • Imechapishwa: 28/05/2020