Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Alimzungumzisha Muusa kwa maneno Yake.

MAELEZO

Hapa wanaraddiwa Jahmiyyah. Majina na sifa Zake hazitengani Naye kutokamana na dhati Yake. Hazina mwanzo wala mwisho, kama ambavo dhati Yake haina mwanzo wala mwisho. Baadhi ya sifa Zake ni za kidhati, nyenginezo ni za kimatendo. Sifa za kimatendo aina yake ni ya kale milele (قديمة النوع), na zinazozuka kutegemea na matukio (حادثة الآحاد).

Baadhi ya sifa za matendo ni maneno. Allaah anazugumza kikweli. Maneno yanasikika kutoka Kwake. Alizungumza na Muusa (´alayhis-Salaam) akayasikia maneno Yake. Anamfunulia Jibriyl ufunuo akayasikia maneno Yake na kisha baadaye akawafikishia Mitume. Kwa hiyo huzungumza anapotaka kwa maneno yanayosikika.

Jahmiyyah wao wanasema kuwa Allaah hazungumzi. Kwa sababu viumbe nao wanazungumza. Tukisema kuwa Allaah anazungumza tutakuwa tumemfananisha na viumbe, ndivo wanavosema.

Hawapambanui kati ya sifa za Muumba na sifa za viumbe. Allaah anazungumza anapotoaka na maneno Yake yanalingana Naye. Sio kama maneno ya viumbe. Maneno Yake ni katika sifa Zake za kimatendo anayosifika nayo akitaka na pale anapotaka na namna anavotaka. Maneno Yake hayana mwanzo wala mwisho, kama zilivyo sifa Zake nyenginezo.

Jahmiyyah wanasema kuwa maneno ya Allaah yameumbwa. Wao wanaona kuwa Allaah aliumba maneno yakazungumza na Muusa, haina maana kwamba Allaah alimzungumzisha Muusa kikweli au kwamba Muusa aliyasikia maneno ya Mola (Subhaanahu wa Ta´ala). Wanasema kuwa Qur-aan imeumbwa na kwamba sio maneno ya Allaah kikweli. Aidha wanaona kuwa Allaah ameiumba Qur-aan katika Ubao uliohifadhiwa ambapo Jibriyl akayachukua kutoka hapo na akampelekea nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah ametakasika kutokamana na wanayoyasema! Allaah kutozungumza ni upungufu juu Yake. Ambaye hazungumzi ni mpungufu. Ndio maana akasema pindi wana wa israaiyl walipomwabudu ndama:

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ ۚ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا ۘ اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ

“Watu wa Muusa walijifanyia, baada kuondoka kwake, katika mapambo yao, umbo la ndama – lilikuwa na sauti kama ya ng’ombe. Je, hawakuona kwamba hawasemezi na wala hawaongozi njia? Walimfanya [kuwa mwabudiwa] na wakawa madhalimu.”[1]

أَفَلَا يَرَوْنَ أَلَّا يَرْجِعُ إِلَيْهِمْ قَوْلًا وَلَا يَمْلِكُ لَهُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا

“Je, hawaoni kwamba [ndama huyo] harejeshi neno na wala hawezi kuwadhuru na wala kuwanufaisha?”[2]

Allaah amekemea kitendo cha Saamiriy aliyeabudiwa na wana wa israaiyl. Walisema:

هَـٰذَا إِلَـٰهُكُمْ وَإِلَـٰهُ مُوسَىٰ فَنَسِيَ

“Huyu ndiye mwabudiwa wenu na mwabudiwa wa Muusa lakini amesahau.”[3]

Ina maana kwamba Muusa amesahau na akaenda kumtafuta Mola wake? Allaah akawakemea na akasema:

أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا ۘ اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ

“Je, hawakuona kwamba hawasemezi na wala hawaongozi njia? Walimfanya [kuwa mwabudiwa] na wakawa madhalimu.”

Bi maana, ambaye hazungumzi hastahiki kuabudiwa. Ni vipi ataabudiwa ilihali hazungumzi, haamrishi, hakatazi wala haendeshi mambo? Allaah ametakasika kutokamana na yale wa nayoyasema.

[1] 7:148

[2] 20:89

[3] 20:88

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 29/07/2021