49. Baadhi ya fadhila za ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh)


Baada yake anafuatia ´Umar al-Faaruuq. Ameitwa al-Faaruuq (mfarikishi) kwa sababu Allaah amefarikisha kupitia yeye baina ya haki na batili. Aliposilimu Uislamu ulitukuka kwa kuingia kwake katika Uislamu. Kabla ya Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) waislamu walikuwa wanyonge na wakijificha katika pango la Arqam. Pindi aliposilimu Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wakatoka nao kuelekea katika Masjid-ul-Haraam. Hapakuwepo yeyote anayewajongelea ilihali wako pamoja na Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Hapo ndipo Allaah aliutukuza Uislamu kupitia wawili hao. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hatukuacha kuwa na nguvu tangu aliposilimu ´Umar.”[1]

Allaah akaupa Uislamu nguvu kupitia yeye. Ndio maana akaitwa al-Faaruuq.

Yeye ndiye khaliyfah wa pili na kadhalika ndiye Swahabah bora baada ya Abu Bakr asw-Swiddiyq kama ilivyo katika al-Bukhaariy na kwenginepo[2]. Wawili hao ndio mawaziri wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bi maana wenye kumshauri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Waziri ni mtu anayemsapoti na kumsaidia mtawala. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا

“… na Tukamjaalia pamoja naye – yaani Muusa – kaka yake Haaruun kuwa waziri.” (25:35)

Kwa sababu Muusa alimuomba Mola Wake na kusema:

وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي هَارُونَ أَخِي اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي

“Nifanyie waziri katika ahli zangu Haaruun ndugu yangu. Nitie nguvu kwaye, na umshirikishe katika jambo langu.” (20:29-32)

Hii ndio kazi ya waziri. Ni ambaye anashiriki katika maoni, anamsaidia mtawala na kumshauri na kumnasihi.

Kwa hiyo Abu Bakr na ´Umar ndio mawaziri wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ambavyo Haaruun ni waziri wa Muusa (´alayhis-Salaam).

[1] al-Bukhaariy (3863) na (3684), “al-Bidaayah wan-Nihaayah” (03/79)

[2] al-Bukhaariy (3662) na Muslim (08) na (2384).