49. Adhkaar za kwenye Rukuu´


Katika nguzo hii alikuwa akisoma aina mbalimbali za adhkaar na du´aa:

1-

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika  Mola wangu, Aliye mtukufu, kutokamana na mapungufu yote.”

Akisema hivo mara tatu[1],

Wakati mwingine akikariri zaidi ya hivyo[2].

Alikuwa mara nyingine anaweza kuisoma mara nyingi kiasi cha kwamba Rukuu´ yake ilikuwa inaweza kuwa ndefu kama kusimama kwake ambapo ndani yake akisoma zile Suurah tatu ndefu “al-Baqarah”, “an-Nisaa´” na “Aal ´Imraan”. Akitamka du´aa na kuomba msamaha kwa uwazi kabisa, kama ilivyotajwa katika swalah ya usiku.

2-

سبحان ربي العظيم و بحمده

“Ametakasika  Mola wangu, Aliye mtukufu, kutokamana na mapungufu yote, na himdi zote ni Zake.”

Akisema hivo mara tatu[3].

3-

سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلائِكَةِ والرُّوح

“Umetakasika sana kutokamana na mapungufu na uchafu[4]; Mola wa Malaika na roho!”[5]

4-

سبحانك اللهم ربنا و وبحمدك,اللهم اغفر لي

“Kutakasika kutokamana na mapungufu ni Kwako ee Allaah, Mola wetu, na himdi zote unastahiki Wewe. Ee Allaah! Nisamehe!”

Alikuwa akiisoma mara nyingi katika Rukuu´ na Sujuud yake na akiitendea kazi Qur-aan[6].

5-

اللهم لك ركعت,و بك آمنت,و لك أسلمت,خشع لك سمعي,و بصري,و مخي,و عظمي,و عصبي

“Ee Allaah! Kwako Wewe nimerukuu. Wewe nimekuamini. Kwako Wewe nimejisalimisha. Usikizi wangu, uoni wangu, ubongo wangu, mifupa yangu na mishipa yangu vimenyenyekea Kwako.”[7]

6-

اللهم لك ركعت و بك آمنت و لك أسلمت و عليك توكلت. أنت ربي. خشع سمعي و بصري و دمي و لحمي و عظمي و عصبي لله رب العالمين

“Ee Allaah! Kwako nimerukuu. Wewe nimekuamini. Kwako Wewe nimejisalimisha. Wewe ndiye nakutegemea. Wewe ndiye Mola wangu. Usikizi wangu, uoni wangu, damu yangu, nyama zangu, mifupa yangu na mishipa yangu vimenyenyekea kwa Allaah, Mola wa walimwengu.”

7-

سُبْحَانَ ذِي الجبروتِ وَالملكوتِ والْكِبْرِياءِ والْعَظَمة

“Ametakasika kutokamana na mapungufu Mwenye utawala, ufalme, ukubwa na utukufu.”[8]

[1] Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, at-Twahaawiy, al-Bazzaar, Ibn Khuzaymah (604) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” kupitia Maswahabah saba. Inawaraddi wale wanaopinga kutozidisha mara tatu akiwemo akiwemo Ibn-ul-Qayyim na wengineo.

[2] Mtu anapata kufikia kupitia zile Hadiyth zilizoweka wazi ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya muda wa kusimama kwake, kurukuu kwake na kusujudu kwake kuwa sawasawa, kama itakavyokuja katika mlango wa kufuata.

[3] Swahiyh. Abu Daawuud, ad-Daaraqutwniy, Ahmad, at-Twabaraaniy na al-Bayhaqiy.

[4] Abu Ishaaq amesema:

”Subbuuh” maana yake Ametakasika kutokamana na mapungufu yote. “Qudduus” maana yake Amebarikika au Ametakasika.”

Ibn Sayyidih amesema:

“Subbuuh na Qudduus ni sifa mbili katika sifa za Allaah, kwa sababu anatukuzwa na kutakaswa kutokamana na mapungufu yote.” (Lisaan-ul-´Arab)

[5] Muslim na Abu ´Awaanah.

[6] al-Bukhaariy na Muslim. Kusema kwamba anaitendea kazi Qur-aan maana yake anatekeleza yale yaliyoamrishwa ndani yake, nayo ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا

”Basi sabihi kwa himdi za Mola wako na muombe msamaha! Hakika Yeye daima ni Mwingi kabisa wa kupokea tawbah.” (110:03)

[7] Muslim, Abu ´Awanah, at-Twahaawiy na ad-Daaraqutwniy.

[8] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

Faida

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kusoma du´aa zaidi ya moja katika Rukuu´ moja? Wanachuoni wametofautiana juu ya hilo. Ibn-ul-Qayyim amechukua msimamo wa kunyamza katika ”Zaad-ul-Ma´aadh” na an-Nawawiy amelijuzisha katika ”al-Adhkaar”. Amesema:

”Ikiwezekana basi bo bora kuzisoma adhkaar zote hizi. Hivyo ndivyo inatakiwa kufanya katika matendo yote.”

Abut-Twayyib Siddiyq Hasan Khaan hakukubaliana naye juu ya hilo na akasema:

”Mtu badala yake anatakiwa kusoma du´aa hii mara hii na du´aa nyingine mara nyingine. Sioni dalili yoyote ya kwamba zichanganywe zote. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akizichanganya katika nguzo moja hiyo hiyo. Lakini alikuwa mara akileta hii na wakati mwingine akileta nyingine. Kufuata ni bora kuliko kuzusha.” (Nuzuul-ul-Abraar (84))

Maoni haya – Allaah akitaka – ndio sahihi zaidi. Lakini imethibiti katika Sunnan namna ambavyo nguzo hii na nyingine zilivyokuwa ndefu hadi iwe inakaribia urefu wa kisimamo. Hivyo yule anayetaka kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kufanya hivo endapo hatotendea maoni ya an-Nawawiy. Ameipokea Ibn Naswr katika ”Qiyaam-ul-Layl” (76) kutoka kwa ´Atwaa´ kupitia kwa Ibn Jurayj. Au kuzikariri zile du´aa ambazo kuna dalili juu ya kuzikariri huko, jambo ambalo ndilo lililo karibu na Sunnah – na Allaah ndiye anajua zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 115-116
  • Imechapishwa: 17/02/2017