48. Wasikilizeni na watiini viongozi wenu wakandamizaji


Aliwaambia Answaar:

“Baada yangu kutakuwepo mapendeleo… “

Aliwaambia nini Answaar waliopigana, waliokuwa na makazi na wakawa na imani, waliopambana na wakaifungua miji?

Leo wamekuja watu wanaokata matunda ya juhudi za Answaar na Muhaajiruun. Wengi wao wameingia katika Uislamu baada ya Ufunguzi. Baadhi katika wao ni Abu Sufyaan na Mu´aawiyah. Baada yao kikaja kizazi chao kilichotumia vibaya mali hizi. Hatumuingizi Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh) katika watu hawa, lakini kulitokea kitu katika dhuluma na ukandamizi kwa Banuu Marwaan. Walikuwa wakichelewesha ´Aswr na wakiziswali swalah baada ya kuingia wakati wake. Kulikuwa kasoro kati yao. Pamoja na haya Maswahabah waliwavumilia. Watu walikuwa wakilalamika kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya umwagaji damu na uporaji wa al-Hajjaaj. al-Hajjaal alikuwa ni muovu zaidi kuliko watawala wa hii leo. Hii leo wako na serikali, sawa mashariki au magharibi. Alikuwa ni mwenye vurugu na mwenye kufuata matamanio yake tu. Alikuwa akimwaga damu. Anas akasema:

“Subirini. Kwani hakika hakutokuja mwaka isipokuwa ulio baada yake ni mbaya zaidi.”

Aliwaamrisha kuwa na subira. Ameyechukua kutoka katika mafundisho na maelekezo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

´Alqamah bin Waa´iyl amesimulia kutoka kwa baba yake ya kwamba Salamah bin Yaziyd al-Ju´fiy amesema ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha nini lau tutapata viongozi wanaotutaka haki zao na wanatunyima haki zetu?”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa mgongo. Akamuuliza tena ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa mgongo. Swali lilikuwa la khatari na yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulipenda. Swali lilikuwa gumu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme nini? asl-Ash´ath bin Qays akamshika mkono na kusema:

“Sikiliza na utii! Hamkukalifishwa jengine zaidi ya kile mlichobebeshwa na wao hawakukalifishwa jengine zaidi ya kile walichobebeshwa.”[1]

Mtu anaweza kufikiri kuwa haya ni maneno ya asl-Ash´ath bin Qays. Hebu tuseme kuwa ni maneno ya asl-Ash´ath bin Qays, lakini Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyakubali. Kwani mnatambua kuwa Sunnah ni maneno, matendo na yale aliyoyakubali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo kuna mapokezi mengine yanayosema ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Sikiliza na utii! Hamkukalifishwa jengine zaidi ya kile mlichobebeshwa na wao hawakukalifishwa jengine zaidi ya kile walichobebeshwa.”

[1] Muslim (1846).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 419-420
  • Imechapishwa: 23/10/2017