41- Wasia kwa wanandoa

Namalizia kwa kuwanasihi wanandoa yafuatayo:

Wasia wa kwanza: Wanasihiane juu ya kumtii Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), kufuata hukumu Zake zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah na wala wasiyatangulizie ufuataji kipofu wala desturi iliozoeleka kwa watu au madhehebu. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Yule mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake, basi kwa hakika amepotoka upotevu wa wazi kabisa.”[1]

Wasia wa pili: Kila mmoja katika wao ashikamane na yale ya wajibu na haki ambazo Allaah amemuwajibishia mmoja kwa mwengine. Kwa mfano mke asimtake mume kulingana naye sawa katika haki zote. Vilevile mwanaume asitumie fursa ya ule uongozi na mamlaka ambayo Allaah amemfadhilisha yeye juu ya mwanamke ambapo akawa akamdhulumu na kumpiga pasi na haki. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Nao [wanawake] wana haki kama ambayo [ya waume zao] iliyo juu yao kwa mujibu wa Shari´ah – na wanaume wana daraja zaidi juu yao. Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[2]

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا

”Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa yale ambayo wanatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao[3], basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni. Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao[4]. ”Hakika Allaah yujuu, Mkubwa kabisa.”[5]

 Mu´aawiyah bin Haydah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni haki zipi za mke ambazo zinamlazimu mmoja wetu?” Akasema: “Amlishe pale atapokula, amvishe pale atapovaa, wala asiukebehi uso[6] na wala asimpige, asimsuse isipokuwa nyumbani[7] – vipi [mtafanya hivo] ilihali mmekwishaingiliana nyinyi kwa nyinyi isipokuwa kwa yale mliyohalalishiwa kwao.”[8]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wafanyao uadilifu watakuwa katika mimbari ya mwangaza upande wa kulia wa mkono wa Allaah – na mikono yote ya Allaah ni ya kuume – wale ambao wanafanya uadilifu katika kuhukumu kwao, familia zao na yale waliyotawalishwa.”[9]

Wote wawili watapoyatambua haya na kuyatendea kazi, basi Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atawapa maisha mazuri na kuendelea kuishi vivyo hivyo midhali watakuwa pamoja katika furaha na raha. Amesema (´Azza wa Jall):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mwenye kutenda mema katika wanamume au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri na Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[10]

Wasia wa tatu: Ni lazima kwa mwanamke kumtii mume wake katika yale anayomuamrisha katika mipaka ya uwezo wake. Haya ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah amemfadhilisha mwanaume juu ya mwanamke, kama ilivyo katika Aayah mbili zilizotangulia:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ

”Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake.”[11]

وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ

”Wanaume wana daraja zaidi juu yao.”[12]

Kumekuja Hadiyth nyingi Swahiyh zinazotilia nguvu maana hii na zinazoweka wazi kabisa haki za mwanamke akiwa ni mtiifu kwa mumewe au si mtiifu. Ni lazima kutaja baadhi yake huenda ndani yake kuna ukumbusho kwa wanawake wa zama zetu hizi. Amesema (Ta´ala):

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ

“Kumbusha, kwani hakika ukumbusho unawafaa waumini.”[13]

Hadiyth ya kwanza: “Si halali kwa mwanamke kufunga… “

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Asifunge mwanamke ilihali mume wake yupo[14] isipokuwa kwa idhini yake – mbali na Ramadhaan – na asimruhusu yeyote kuingia nyumbani kwake isipokuwa kwa idhini yake.”[15]

Hadiyth ya pili: “Mwanamume atapomwita mke wake kitandani[16] na asije na akalala hali ya kumghadhibikia, basi Malaika wanamlaani mpaka kupambazuke.”[17]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… mpaka mwanamke huyo arudi.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… mpaka mume wake awe radhi naye.”

Hadiyth ya tatu: “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake. Mwanamke atakuwa si mwenye kutekeleza haki ya Mola Wake mpaka kwanza atekeleze haki ya mume wake kiasi cha kwamba endapo atamtaka akiwa juu ya tandiko la farasi, basi hatakiwi kumkatalia.”[18]

Hadiyth ya nne: “Mwanamke hatomuudhi mume wake hapa duniani isipokuwa husema mke wake katika al-Huur al-´Ayn: “Usimuudhi! Allaah akulaani! Kwani yeye kwako ni mgeni na anakaribia kukuacha na kuja kwetu.”[19]

Hadiyth ya tano: Huswayn bin Muhswan ameeleza: “Shangazi yangu amenihadithia akisema: “Nilienda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikiwa ni mwenye kuhitajia baadhi ya haja ambapo akasema: “Je, wewe una mume?” Nikajibu: “Ndio.” Akasema: “Uko vipi na kwake?” Nikajibu: “Sina upungufu katika kumtii na kumhudumia isipokuwa yale yanayonishinda.” Akasema: “Angalia vizuri uhusiano wako kwake! Kwani yeye ndiye ufunguo wako wa Pepo na wa Moto.”[20]

Hadiyth ya sita: “Ataposwali mwanamke [vipindi vyake] vitano, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, basi ataingia katika mlango wa Pepo wowote anaoutaka.”[21]

[1] 33:36

[2] 02:228

[3] Bi maana kutoka katika utiifu. Ibn Kathiyr amesema:

an-Nushuuz ni kule kujinyanyua. Mwanamke mwenye tabia hii ni yule mwenye kujinyanyua juu ya mume wake, anayaacha maamrisho yake na anampuuza.”

[4] Bi maana mwanamke atapomtii mume wake katika yale yote ambayo anayataka ambayo Allaah ameruhusu, basi hana sababu yoyote kwake baada ya yote hayo na hana haki ya kumpiga wala kumsusa. Maneno Yake:

إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا

”Hakika Allaah yujuu, Mkubwa kabisa.”

Haya ni matishio kwa mwanaume akimdhulumu mwanamke pasi na sababu. Basi atambue kuwa Allaah ndiye yujuu, Mkubwa kabisa. Yeye [Allaah] ndiye atamlipia yule mwenye kumdhulumu.” Hivi ndivyo ilivyotajwa katika “Tafsiyr” ya Ibn Kathiyr.

[5] 04:34

[6] Asiseme: “Allaah aukebehi uso wako!”. Maneno yake:

“… wala asimpige… “

kunamaanishwa kupiga uso. Wakati wa haja kunapigwa kwengine mbali na uso.

[7] Asimhame isipokuwa katika malazi na wala asimkimbie na kwenda katika nyumba nyingine. Hivi ndivyo ilivyotajwa katika “Sharh-us-Sunnah” (01/26/03).

[8] Ameipokea Abu Daawuud (01/334), al-Haakim (02/178-188), Ahmad (03/05) na ziada ni yake kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. al-Haakim amesema: “Swahiyh” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[9] Ameipokea Muslim (07/06), al-Husayn, al-Marwaziy katika “az-Zawaa-id” ya Ibn-ul-Mubaarak (02/120) kutoka katika al-Kawaakib ya Ibn ´Urwah al-Hanbaliy mjaladi nambari. 575, Ibn Mandah katika “at-Tawhiyd” (01/94) ambaye amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh.”

[10] 16:97

[11] 04:34

[12] 02:228

[13] 51:55

[14] Yupo katika mji. an-Nawawiy amesema katika “Sharh Muslim” (07/115) chini ya Hadiyth ya pili:

“Makatazo haya ni kwa njia ya uharamu. Wameweka wazi wenzetu.”

Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi kama ilivyo katika “al-Fath” na inatiliwa nguvu na upokezi wa kwanza. an-Nawawiy anaendelea kusema:

“Hilo ni kwa sababu mume ana haki ya kustarehe naye katika siku zote. Haki yake ni ya uwajibu papo kwa hapo. Kwa hivo asikose haki yake kwa mambo ya kujitolea [sunnah] au ya wajibu ambayo mtu amejiwajibishia.”

Ikiwa ni wajibu kwa mwanamke kumtii mume wake katika kutekeleza matamanio yake kwake, basi kinachosika msitari wa mbele ni kwamba ni wajibu kwake kumtii katika yale ambayo ni muhimu zaidi kuliko hayo; nacho si kingine ni kuwalea watoto wake, kutengeneza familia yake na mfano wa hayo katika haki na mambo mengine ya wajibu.”

al-Haafidhw amesema katika “al-Fath”:

“Katika Hadiyth tunapata kujifunza ya kwamba haki ya mume imesisitizwa zaidi kuliko mambo ya sunnah. Kwa sababu haki yake mume ni ya wajibu na kutekeleza wajibu ni jambo linatangulizwa kabla ya mambo yaliyopendekezwa.”

[15] Ameipokea al-Bukhaariy (04/42) kwa mapoeki ya kwanza, Muslim (03/91) kwa mapokezi ya pili, Abu Daawuud (01/385), an-Nasaa´iy katika “al-Kubraa” (02/63) na ziada ni ya hao wawili. Mlolongo wa wapoezi wake ni mzuri na uko kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim. Vilevile ameipokea Ahmad (02/316), at-Twahaawiy katika “al-Mushkil” (02/425), Abush-Shaykh katika “Ahaadiyth Abiyz-Zubayr” (126) kupitia njia ya Abu Hurayrah na kwa Ahmad katika upokezi wenye maana ya nyongeza.

[16] Hiki ni kinaya cha jimaa. Hilo linatiliwa nguvu na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtoto [wa mtu] ni yule wa kitandani.”

bi maana yule aliyempata mtu kwa kufanya jimaa kitandani. Katika Qur-aan na Sunnah kuna mambo mengi yaliyotajwa kwa njia ya kinaya kwa sababu ni mambo yanaonewa haya na wengi. Hayo yamesemwa na Ibn Abiy Jamrah, kama ilivyo katika “Fath”.

[17] Ameipokea al-Bukhaariy (04/241), Muslim (04/157) na upokezi mwingine ni wake, Abu Daawuud (01/334), ad-Daarimiy (02/149), Ahmad (02/225) na upokezi wa pili ni wake pia na ad-Daarimiy.

[18] Hadiyth ni Swahiyh. Ameipokea Ibn Maajah (01/570), Ahmad (04/381) kutoka kwa ´Abdullaah bin Abiy Awfaa, Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake, al-Haakim kama ilivyokuja katika “at-Targhiyb” (03/76) na ametaja upokezi unaousapoti kutoka kwa Zayd bin Arqam na akasema:

“Ameipokea at-Twabaraaniy kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.”

 Nimeipokea katika “as-Swahiyhah” (173).

[19] Ameipokea at-Tirmidhiy (02/208), Ibn Maajah (01/621), Haytham bin Kaliyb katika “al-Musnad” yake (01/167/05), Abul-Hasan at-Twuusiy katika “al-Mukhtaswar” yake (02/119/01) na wengineo.

[20] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (01/47/07), Ibn Sa´d (08/459), an-Nasaa´iy katika “´Ishrat-un-Nisaa´”, Ahmad (04/341), at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” (01/170) kutoka katika “Zawaa-id” yake, al-Haakim (02/189) na wengineo.

[21] Hadiyth ni nzuri au Swahiyh. at-Twabaraaniy  ameipoke akatika “al-Awsatw” (02/169) kwa mujibu wa mpangilio wake, Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah kama ilivyo katika “at-Targhiyb” (03/73), Ahmad (1661) kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Abu Nu´aym (06/308), al-Jurjaaniy (291) kupitia kwa Anas bin Maalik.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 279-286
  • Imechapishwa: 20/05/2018