1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayemuomba udhuru ndugu yake na asimkubalie [udhuru wake], basi atakuwa na mfano wa dhambi ya afisa wa forodha.”

Hadiyth ni nzuri.

 2 – Ni wajibu kwa mwenye busara kukubali udhuru wa ndugu yake kwa kosa la lililopita au upungufu na ajaalie kama hakufanya kosa lolote. Kwa sababu nachelea yule asiyekubali nyudhuru basi hatofikia hodhi ya Mteuliwe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule mwenye kuzembea kwa sababu fulani basi ni lazima kumuomba udhuru nduguye kwa sababu ya kuzembea kwake.

3 – Haifai kumuomba ndugu yako udhuru kwa wingi. Kuomba udhuru kwa wingi kunapelekea kudhaniwa vibaya. Napendekeza kufanya uchache kuomba udhuru kwa jumla. Natambua kuwa nyudhuru huchanganyikana na uwongo. Ni wachache nimewaona wakiomba udhuru pasi na kuchanganya nyudhuru zao na uwongo. Ambaye amekubali kosa basi anastahiki kusamehewa. Udhalilifu wa kuomba udhuru juu ya kosa hufanya hasira zikapungua.

4 – Abu Qilaabah amesema:

“Ukifikiwa na khabari juu ya ndugu yako kuhusu kitu unachokichukia basi mtafutie udhuru. Usipompatia udhuru basi sema: “Pengine ana udhuru nisioufahamu.”

5 – Haifai kwa mtu kutangaza adhabu kwa mtu ambaye hakuweka hadharani dhambi yake. Ambaye anapewa udhuru ima akawa ni mkweli au mwongo. Kama ni mkweli basi amestahiki kusamehewa. Waovu kabisa katika watu ni wale wasioficha makosa. Na kama ni mwongo basi ni wajibu kwa yule anayetambua kuwa anasema uwongo pamoja na hivyo anajidharaulisha kwa kutafuta udhuru asimuadhibu kwa dhambi yake iliyotangulia. Badala yake amshukuru kwa kitendo chake chema kilichoko katika udhuru wake. Sio aibu kwa yule anayeomba msamaha akajidhalilisha na kunyenyekea mbele ya ndugu yake wakati anapoomba msamaha.

6 –  Kuombana udhuru kunaondosha masononeko, huzuni, chuki na woga. Kuombana udhuru mara chache kunazamisha matendo ya jinai makubwa na makosa mengi. Kuombana udhuru mara nyingi kunapelekea kufikiriwa vibaya na maoni mabaya. Lau udhuru usingelikuwa na sifa nyingine nzuri isipokuwa kwamba yule anayeomba udhuru na msamaha hajioni nafsi yake basi ingelikuwa inatosha kwa yule mwenye busara kukubali udhuru na msamaha wakati wa kila kosa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 182-186
  • Imechapishwa: 16/08/2021