14 – Mwanamke mwenye hedhi akipiga kiguzo cha ´Aqabah na akapunguza nywele zake, basi atatoka kwenye Ihraam yake na vitahalalika kwake vile vilivyokuwa haramu juu yake katika Ihraam. Isipokuwa tu mume wake hatohalalika kwake. Haijuzu kwake kujimakinisha kwa mume wake mpaka kwanza atufu kwenye Ka´bah Twawaaf-ul-Ifaadhwah. Akimjamii katika kipindi hichi basi atalazimika kutoa fidia; kuchinja kondoo Makkah na ataigawa kuwapa masikini wa Haram. Kwa sababu wamefanya hayo baada ya Tahallul ya kwanza.

15 – Mwanamke akipatwa na hedhi baada ya Twawaaf-ul-Ifaadhwah, basi asafiri anakotaka na itadondoka kwake Twawaaf-ul-Wadaa´. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Swafiyyah bint Huyay alipatwa na hedhi baada ya Twawaaf-ul-Ifaadhwah. Nikamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Je, ni mwenye kutuzuia?” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Amekwishafanya Twawaaf-ul-Ifaadhwah na akatufu kwenye Ka´bah kisha ndio akapata hedhi baada ya Twawaaf-ul-Ifaadhwah.” Akasema:

“Basi aende zake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas amesema:

“Watu wameamrishwa ahadi yao ya mwisho iwe kuzunguka Ka´bah; isipokuwa tu imekhafifishwa kwa mwanamke mwenye hedhi.”

Ibn ´Abbaas amesimulia pia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Amemruhusu mwanamke kuondoka kabla ya kutufu Ka´bah ikiwa amekwishatufu Twawaaf-ul-Ifaadhwah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” amesema:

“Ibn-ul-Mundhir amesema: “Hayo ndio yamesemwa na wanachuoni wote akiwemo Maalik, al-Awzaa´iy, ath-Thawriy, Ahmad, Ishaaq, Abu Thawr, Abu Haniyfah na wengineo:”[1]

Mtunzi wa “al-Mughniy”amesema:

“Haya ndio maoni ya Fuqahaa´ wote wa miji na akasema: “Hukumu za damu ya uzazi ni kama hukumu za hedhi. Kwa  sababu hukumu za damu ya uzazi ndio hukumu za hedhi katika yale yanayopasa na yanayodondoka.”[2]

[1] (08/218).

[2] (03/461).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 14/11/2019