48. Baadhi ya fadhilah za Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh)

Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye mbora katika makhaliyfah. Allaah amemsifu pale aliposema:

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ

“Wala wasiape wale wenye fadhilah miongoni mwenu na nafasi kuwa hawatowapa [swadaqah] jamaa wa karibu.” (24:22)

Aayah hii imeshuka juu ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipoapa kuwa hatompa Mistwha bin Uthaathah kitu katika mali. Mtu huyu alikuwa ni ndugu ambaye alikuwa akimpa matumizi. Pindi alipodanganyika na wale waliozungumza machafu na akawasadikisha na yeye akawa ameongea, ndipo Abu Bakr akamghadhibikia na akaapa kuwa hatompa. Allaah akashusha Aayah ifuatayo:

وَلَا يَأْتَلِ

“Wala wasiape… “

أُولُو الْفَضْلِ

“… wale wenye fadhilah.”

Akamsifu Abu Bakr kuwa ni katika watwenye fadhilah.

Katika Aayah nyingine imekuja:

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ

“Msipomnusuru basi Allaah amekwishamnusuru, pale walipomtoa wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili.”

Wawili hawa ni watu gani? Ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Abu Bakr. Haya ni kwa maafikiano.

إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Wawili hao walipokuwa katika pango, alipomwambia swahiba yake: “Usihuzunike – hakika Allaah yupamoja nasi.” (09:40)

Amemthibitishia usuhuba pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Abu Bakr ndiye Swahabah bora. Kadhalika ndivyo zinavyofahamisha Hadiyth Swahiyh zinazopatikana katika al-Bukhaariy na kwenginepo. Mbora katika Ummah huu ni Abu Bakr asw-Swiddiyq. Hilo ni kwa sababu ya kutangulia kwake katika Uislamu, kumnusuru kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kulazimiana naye.

Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki Ummah mzima uliafikiana juu ya kumchagua Abu Bakr. Pindi waliporitadi walioritadi katika mabedui ambaye aliwasimamia kidete na akapambana nao ni Abu Bakr mpaka Allaah akaithibitisha dini hii na akawasambaratisha walioritadi kupitia yeye. Fadhilah zake ni nyingi (Radhiya Allaahu ´anh). Anaitwa “as-Swiddiyq” (mkweli mno). Daraja ya wakweli inakuja baada ya daraja ya Mitume. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha miongoni mwa Manabii, na wakweli, na mashahidi na waja wema  – na uzuri ulioje hao kuwa ni rafiki!” (04:69)

asw-Swiddiyq ni ambaye anasema ukweli sana. Ni mtu amepindukia katika ukweli. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatoacha mtu kuendelea kusema ukweli na kuchunga ukweli mpaka aandikwe mbele ya Allaah kuwa ni “mkweli”.”[1]

[1] al-Bukhaariy (6094) na Muslim (102) na (2606)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 115-117
  • Imechapishwa: 10/01/2024