Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Unafiki ni ukafiri na maana yake ni kumkufuru Allaah, kumuabudu mwengine asiyekuwa Yeye na wakati huohuo mtu akaonyesha Uislamu waziwazi. Hivyo ndivyo walivyofanya wanafiki wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

MAELEZO

Mnafiki anaficha ukafiri na anaonyesha Uislamu. Allaah ameteremsha juu ya wanafiki Aayah nyingi katika Suurah “at-Tawbah”, “al-Ahzaab” na “al-Munaafiquun”.

Unafiki umegawanyika aina mbili:

1- Unafiki wa kimatendo. Unafiki huu haumtoi mtu katika Uislamu na ni kama madhambi mengine makubwa. Umetajwa katika Hadiyth:

“Alama za mnafiki ni tatu; anapoongea anasema uongo, anapoahidi anakhalifu na anapoaminiwa anafanya khiyana.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… anapoahidi anafanya udanganyifu… “

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… anapogombana, huapiza… “[2]

2- Unafiki wa kimaneno. Unafiki huu mtu anaonyesha Uislamu na anaficha ukafiri. Hivo ndivyo walivyokuwa wakifanya wale wanafiki waliokuweko wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowashinda Quraysh katika vita vya Badr makafiri wakaambizana wamuonyeshe Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake kuwa wako pamoja nao na wafiche dini yao. Huu ni unafiki wa kiimani.

[1] al-Bukhaariy (33) na Muslim (59).

[2] al-Bukhaariy (34) na Muslim (58).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 160-161
  • Imechapishwa: 05/06/2019