47. Tofauti iliyopo kuhusu ni nani bora kati ya ´Uthmaan na ´Aliy

Tumetangulia kuzungumza juu ya fadhilah za Maswahabah na kwamba wanatofautiana katika ubora baina yao. Hata hivyo wanashirikiana katika fadhilah za uswahabah. Hakuna yeyote anayeshirikiana nao katika fadhilah hii. Hakuna yeyote anayewafikia katika hili. Kuhusu wao kati yao wanashindana. Baadhi ni wabora zaidi kuliko wengine. Tukisema kuwa baadhi ni wabora zaidi kuliko wengine haina maana kwamba tuwatukane wale wenye kushindwa ubora. Haijuzu kumtukana yule anayeshindwa ubora ilihali ni Swahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kadhalika tumetangulia kubainisha kuwa Maswahabah bora ni wale makhaliyfah wanne. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangofu na wenye kuongozwa baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu.”

Ambaye amewaita kuwa ni ´makhaliyfah waongofu` ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pia akaamrisha kushikamana na Sunnah zao kwa kuwa wanapita juu ya Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanazithibitisha na kuzitawanya kutokana na ile elimu, nguvu na uongozi aliyowapa Allaah.

Mbora zaidi katika makhaliyfah wanne ni Abu Bakr na kisha ´Umar. Haya ni kwa maafikiano ya waislamu. Walitafautiana kwa ´Aliy na ´Uthmaan ni nani ambaye ni bora zaidi. Kuna kundi lilimfadhilisha ´Uthmaan. Kundi jengine likamfadhilisha ´Aliy. Kundi jengine halichukua msimamo wowote. Yote haya yanahusiana na ubora na fadhilah. Kuhusu uongozi Ummah mzima umeafikiana juu ya kwamba uongozi baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wa Abu Bakr, kisha wa ´Umar, halafu wa ´Uthmaan na kisha wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Huu ndio mpangilio wa uongozi kwa maafikiano. Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”:

“Mwenye kutukana uongozi wa mmoja katika hawa ni mpotevu zaidi kuliko punda wa kufugwa.”[1]

Kuna tofauti kati ya suala la ubora na suala la uongozi. Kuhusu suala la ubora waislamu wameafikiana juu ya kwamba mbora ni Abu Bakr na kisha ´Umar. Wakatafautiana ni nani bora kati ya ´Aliy na ´Uthmaan. Maoni sahihi ni kwamba ´Uthmaan ndiye bora zaidi. Kwa mtazamo wa kuwepo tofauti inatajwa. Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye bora zaidi. Dalili ni kuwa watu wa mashauriano walimtanguliza ´Uthmaan juu ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) katika uongozi.

Suala la ubora kati ya ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ni kitu chepesi. Kutukana uongozi ndio upotofu. Kwa sababu Raafidhwah wanasema kuwa khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ´Aliy na ndiye aliyeachiwa wasia. Wanasema kuwa Maswahabah walimdhulumu na wakampora uongozi. Isitoshe wanamlaani Abu Bakr na ´Umar na wanawaita kuwa ni ´masanamu mawili ya ki-Quraysh`. Hili bila ya shaka yoyote ni upotevu, ukafiri na ni kwenda kinyume na maafikiano. Khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, halafu ´Umar, halafu ´Uthmaan na halafu ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] Tazama “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”, uk. 193 Sharh ya mtunzi (Hafidhwahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 114-115
  • Imechapishwa: 10/01/2024