2- Unafiki umegawanyika aina mbili:

Aina ya kwanza: Unafiki wa kiimani. Huu ni ule unafiki mkubwa ambao mwenye nao anaonyesha Uislamu na anaficha ukafiri. Aina hii inamtoa mtu nje ya dini kikamilifu na mwenye nao ni mwenye kuwekwa kwenye shimo la chini kabisa Motoni. Allaah amewaeleza wenye nao kwa sifa zote za ukafiri na kwamba wana ukafiri na hawana imani yoyote, kufanya istihzai na dini na  wenye nao, kuwafanyia maskhara na kumili kikamilifu kwa maadui wa dini kwa kushirikiana nao juu ya kuufanyia uadui Uislamu. Watu aina hii wako katika kila wakati na khaswa pindi kunapodhihiri nguvu za Uislamu na hawawezi kukabiliana nazo kiunje. Hivyo matokeo yake wanadhihirisha kuingia ndani yake kwa minajili ya kuufanyia vitimbi na kuwafanyia watu kwa undani. Sababu nyingine ili waweze kuishi pamoja na waislamu na waisalimishe damu na mali yao. Hapo ndipo mnafiki hudhihirisha imani yake juu ya Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya mwisho ilihali ndani ya moyo hana chochote katika hayo na anayakadhibisha na hamwamini Allaah na wala haamini ya kwamba Allaah amezungumza kwa maneno aliyoyateremsha kwa watu aliowafanya kuwa wajumbe kwa watu wawaongozao kwa idhini Yake na kuwaonya na kuwakhofisha adhabu ya Yake.

Allaah ameivunja sitara ya wanafiki hawa, akafichua siri zao ndani ya Qur-aan tukufu na akawawekea wazi waja mambo yao ili wao na watu wao wafanye tahadhari. Ametaja kwamba kuna makundi aina tatu ya watu mwanzoni mwa al-Baqarah:

1- Waumini.

2- Makafiri.

3- Wanafiki.

Baada ya hapo akataja Aayah nne juu ya waumini, Aayah mbili juu ya makafiri na Aayah kumi juu ya wanafiki. Hayo ni kwa sababu ya wingi wao na ujumla wa kujaribiwa nao na ukubwa wa fitina yao juu ya Uislamu na waislamu. Hakika mitihani ya Uislamu juu yao ni mikubwa sana. Kwa sababu wanajinasibisha juu yake, kuunusuru na kuupenda ilihali ukweli wa mambo wao ni maadui wa huo Uislamu. Wanautoa uadui wao kwa kila namna kiasi cha kwamba mjinga asiyefahamu anafikiria kuwa elimu na kutengeneza. Ni ujinga na ufisadi uliopindukia.

Unafiki aina hii umegawanyika sampuli sita[1]:

1- Kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2- Kuyakadhibisha baadhi ya aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

3- Kumchukia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

4- Kuyachukia baadhi ya aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

5- Kufurahishwa na kuanguka dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

6- Kuchukia dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushinda.

[1] Majmuu´-ut-Tawhiyd an-Najdiyyah, uk. 09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 17/03/2020