Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka vitanga vyake vya mikono juu ya magoti yake[1] na akawaamrisha Maswahabah kufanya vivyo hivyo[2]. Alimwamrisha vilevile yule mtu aliyeswali vibaya kufanya hivo kama tulivyotangulia kutaja punde.

Alikuwa akimakinisha mikono yake juu ya magoti yake kama vile ameyashikilia[3].

Alikuwa akitenganisha kati ya vidole vyake[4]. Alimwamrisha hivo yule mtu mwenye kuswali makosa na kusema:

“Unaporukuu basi viweke vitanga vya mikono yako juu ya magoti yako, tenganisha kati ya vidole vyako kisha ubaki hivyo mpaka kila kiungo cha mwili kitue pahali pake.”[5]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akijitawanya na akitenganisha visugudi vyake na mbavu zake[6].

Wakati anapoenda katika Rukuu´ anautandaza na kuuweka sawa mgongo wake[7]. Kiasi cha kwamba iwapo mtu angelimwaga maji juu ya mgongo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yangelitulia[8]. Alimwambia mtu yule aliyeswali kimakosa:

“Unapoenda katika Rukuu´ basi weka vitanga vyako vya mikono juu ya magoti yako, unyooshe mgongo wako na tulizana kwenye Rukuu´ yako.”[9]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakiinamishi kichwa chake na wala hakiinui[10] isipokuwa kilikuwa baina yake.

[1] al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

[3] al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[4] at-Twayaalisiy na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Imetajwa katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (809).

[5] Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” zao.

[6] at-Tirmidhiy aliyeisahihisha na Ibn Khuzaymah.

[7] al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh na al-Bukhaariy.

[8] at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” na ”al-Mu´jam as-Swaghiyr”, ´Abdullaah bin Ahmad katika ”Zawaa-id-ul-Musnad” na Ibn Maajah.

[9] Ahmad na Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[10] Abu Daawuud na al-Bukhaariy katika ”Juz-ul-Qiraa-ah” kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Maana ya hakiinui kichwa chake ina maana kwamba hakinyanyui zaidi ya kichwa chake mpaka kikawa juu zaidi ya mongo. Tazama ”an-Nihaayah”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 17/02/2017