1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hatoingia Peponi mmbea.”

2 – Ni lazima kwa watu wote kuacha mambo yanayopelekea katika chuki, magomvi na mipasuko kati ya watu. Aliye na busara haingii ndani ya tuliyoyataja. Hakubali maneno ya mmbea kwa hali yoyote. Anajua ni dhambi gani alionayo mmbea huko Aakhirah.

3 – Sulaymaan bin Daawuud (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee mwanangu kipenzi! Nakutahadharisha na umbea. Hakika ni mkali zaidi kuliko panga.”

4 – ´Amr bin Maymuun amesema:

“Pindi Muusa alipotaka kumuona Mola wake akamuona bwana mmoja chini ya ´Arshi nafasi ambayo yeye pia alikuwa anaitaka. Akamuuliza Mola wake amweleze jina lake, lakini Akasema: “Nitakweleza badala yake sifa zake tatu. Alikuwa hawahusudu watu kwa yale ambayo Allaah amewapa kutokana na fadhilah Zake. Hakuwa na utovu wa nidhamu kwa wazazi. Alikuwa si mwenye kueneza umbea.”

5 – al-´Utbiy amesema:

“Nilimsikia mwanamke wa kibedui mmoja akimuusia mwanae: “Lazimiana na kuchunga sira na tahadhari kutokamana na umbea. Kwani umbea hauachi mapenzi isipokuwa huyaharibu wala chuki isipokuwa huiwasha.”

6 – Ni lazima kwa anayetambulika kwa umbea aepukwe. Kusiaminiwe mapenzi yake. Asiweko yeyote atakayefanya naye mawasiliano wala kuishi naye.

7 – Ibraahiym bin Abiy ´Ublah amesema:

“Nilikuwa nimeketi na Umm-ud-Dardaa´ wakati alipokuja mtu na kusema: “Ee Umm-ud-Dardaa´! Kuna mtu amekusema vibaya mbele ya ´Abdul-Malik bin Marwaan.” Akasema: “Tunatuhumiwa kwa uwongo na kutakaswa kwa kitu ambacho hatukufanya.”

8 – Ni wajibu kwa mwenye busara kupuuza tetesi za mmbea na kuyageuza yote hayo katika mkabala mzuri na kuepuka yote yasiyoendana na wenye busara.

9 – Yahyaa bin Abiy Kathiyr amesema:

“Anayowahi kufanya mmbea katika saa moja hayafanywi ndani ya mwezi mmoja.”

10 – Miongoni mwa maafaa ya umbea ni kwamba unavunja pazia, unarithisha chuki, unaondosha mapenzi, unafanya upya uadui, unapasua mshikano, unachochea chuki na kuongeza machukizo. Anayefikiwa na khabari kwamba nduguye amefanya kitu basi anatakiwa kumkosoa na kukubali udhuru wake akiomba udhuru. Hata hivyo asikithirishe kumkosoa. Aidha anatakiwa kuhakikisha anashukuru pindi inapohifadhiwa haki ya mtu, kusubiri wakati inapokiukwa na kukosoa pindi inapo anapokabiliwa vibaya.

11 – Ni wajibu kwa aliye na busara kutozembea kumkosoa ndugu yake juu ya kosa lake. Kwa sababu yule asiyekosoa wakati wa kosa anakuwa si mwenye kuhifadhi yale mapenzi.

12 – Ni bora kukosoa kuliko chuki iliyojificha ndani. Kukosoa kunaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko kupuuzilia mbali.

13 – Mwenye busara hatakiwi kukosoa kwa wingi. Kwani kunachelewa mkosolewa akarudi kwa yale aliyokosolewa. Yule anayemkosoa ndugu yake kwa kila kosa kwa kweli atamchosha na kumfanya aanze kumchukia. Ni vibaya kukosoa kwa wingi. Vivo hivyo ni miongoni mwa utovu wa adabu uliomkubwa kule kuacha kukosoa. Kukosoa kwa wingi kunaua mapenzi na kutisha.

14 – ´Aliy bin Abiy Twaalib amesema:

“Usikosoe kwa wingi. Ukosoaji unapelekea katika chuki na bughudha na tabia mbaya.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 176-182
  • Imechapishwa: 15/08/2021