Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili. Nako ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga na shirki na watu wake.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi mitatu ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili. Kwa msemo mwingine ina maana kwamba mtu aijue dini ya Kiislamu kwa dalili zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Dini ya Kiislamu au ukitaka pia sema Uislamu maana yake ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga na shirki na watu wake. Kwa nji hii imekusanya mambo hayo matatu.

Mja kujisalimisha kwa Mola Wake maana yake ni kujisalimisha ambako kumewekwa katika Shari´ah. Huko inakuwa kwa kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) na kumwabudu Yeye pekee. Aina hii ndio ambayo mtu anasifiwa na kulipwa thawabu kwao. Ama kuhusu ujisalimishaji wa kilimwengu, mtu hapewi thawabu kwa jambo hilo, kwa sababu mtu hana njia ya kukwepa ujisalimishaji aina hii.  Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ

“… na hali Kwake amejisalimisha kila aliye katika mbingu na katika ardhi akipenda asipende na Kwake watarejeshwa.” (Aal ´Imraan 03 : 83)

Kunyenyekea Kwake kwa kumtii – Kunakuwa kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Utiifu maana yake ni kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake.

Kujitenga na shirki na watu wake – Maana yake ni mtu ajiweke mbali na shirki na ajiepushe nayo, jambo ambalo linalazimisha vilevile kujitenga mbali na watu wake. Allaah (Ta´ala) amesema:

قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ

“Kwa hakika mna kigezo chema kwa Ibraahiym na wale walio pamoja naye walipowaambia watu wao: “Hakika Sisi tumejitenga mbali nanyi na yale yote mnayoyaabudu badala ya Allaah, tunakukanusheni na umedhihirika baina yetu na baina yenu uadui na bughudha daima mpaka mumuamini Allaah pekee.” (al-Mumtahinan 60 : 04)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 68
  • Imechapishwa: 28/05/2020