42- Haijuzu kuchupa mpaka katika sanda wala kuzidisha zaidi ya mashuka matatu. Kwa sababu ni jambo linalokwenda kinyume na yale aliyokafiniwa ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyotangulia katika masuala yaliyotangulia. Isitoshe kufanya hivo ni kuharibu mali, jambo lililokatazwa na khaswa kwa kuzingatia kwamba waliohai wana haki nayo zaidi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah anachukia kwenu mambo matatu, porojo, kuharibu mali na kuulizauliza/kuombaomba.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/266), Muslim (05/131), Ahmad (04/246, 249, 250, 254) kutoka katika Hadiyth ya al-Mughiyrah bin Shu´bah.

Hadiyth hii ina ushahidi mwingine kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Ameipokea Muslim.

Kwa mnasaba huu napendezwa na yale yaliyosemwa na ´Allaamah Abut-Twayyib “ar-Rawdhwat-un-Nadiyyah” (01/165):

“Kitendo cha kuzifanya sanda zikawa nyingi na kuchupa katika thamani yake ni jambo lisilopendeza. Kwa sababu kama lisingepokelewa katika Shari´ah basi ingelikuwa ni katika kuharibu mali. Kwa sababu ni kitu asichonufaika kwacho maiti na wala manufaa yake hayamrudilii maiti. Allaah amrehemu Abu Bakr as-Swiddiyq pale aliposema: “Hakika aliyehai ndiye ana haki zaidi ya vipya.” Aliyasema hayo wakati alipolenga moja katika nguo zake iwe ni sanda yake ambapo akaambiwa:

“Hii ni kuukuu.”

43- Mwanamke katika hilo ni kama mwanaume. Kwani hakuna dalili inayofarikisha[1].

Kuhusu Hadiyth ya Laylah bint Qaaif ath-Thaqafiyyah katika kumkafini msichana wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mashuka matano cheni ya wapokezi wake si yenye kusihi. Kwa sababu ndani yake yumo Nuuh bin Hakiym ath-Thaqafiy, naye hajulikani. Hayo yamesemwa na al-Haafidhw Ibn Hajar na wengineo. Kuna kasoro nyingine iliyobainishwa na az-Zayla´iy katika ”Naswb-ur-Raayah” (02/258).

Mfano wake ni yale yaliyozidishwa na baadhi yao katika kisa cha kuoshwa kwa msichana wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliyokwishatangulia katika ukurasa wa 48 kwa tamko:

“Tukamvika sanda katika mashuka matano.”

ni shadhah au munkari. Hayo nimeyahakiki katika “adh-Dhwa´iyfah” (5844).

[1] Hadiyth inayosema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivikwa sanda kwa mashuka saba ni munkari. Amepwekeka nayo yule mwenye kusifiwa kuwa hifdhi mbaya. Irejee katika ”Naswb-ur-Raayah” (02/261-262).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 26/02/2020