47. Majina ya Allaah mazuri mno na sifa Zake kuu kabisa


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Anayo majina mazuri mno na sifa kuu kabisa.

MAELEZO

Amesema (Ta´ala):

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ

“Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye. Anayo majina mazuri kabisa.”[1]

Majina Yake tote ni mazuri mno kwa sababu yanajulisha ukamilifu na yana maana kubwakubwa. Kila jina limebeba sifa kubwa ya Allaah (´Azza wa Jall). Sio majina makavumakavu yasiyokuwa na maana. Majina Yake yote yako na maana kubwakubwa. Ndio maana yakawa mazuri mno. Mwingi wa huruma linajulisha huruma. Mwenye kusikia linajulisha usikizi. Mwenye kuona linajulisha uoni. Mwenye kujua linajulisha ujuzi. Aliye hai linajulisha uhai na kadhalika.

Sifa Zake zote ni kuu kabisa. Sio kama sifa za viumbe ambazo zinaweza kuwa zenye kusimangwa.

[1] 20:8

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 39
  • Imechapishwa: 29/07/2021