47. Hekima ya tatu ya swawm: Kuushughulisha moyo kumtaja Allaah

Miongoni mwa hekima za funga ni kwamba moyo unajishughulisha kufikiri na kumtaja Allaah. Kwa sababu kufanya mambo ya matamanio kunapelekea upumbaaji. Si hayo tu pengine vilevile jambo hilo likapelekea kuufanya moyo kuwa susuwavu na kuupofoa kutokamana na haki. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaelekeza kufanya uchache wa vyakula na vinywaji. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hajapatapo mwanadamu kujaza chombo kibaya zaidi kuliko tumbo. Inatosha kwa mwadamu [kula] matonge kadhaa kwa ajili ya kuunyoosha mgongo wake. Akiwa hana budi, basi theluthi iwe ya chakula chake, theluthi iwe ya kinywaji chake na theluthi iwe kwa ajili ya pumzi.”

Ameipokea Ahmad, an-Nasaa´iy na Ibn Maajah[1].

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kwamba Handhwalah al-Usaydiy – ambaye alikuwa ni mmoja wa waandishi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Handhwalah amefanya unafiki.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kivipi?” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tunakuwa kwako ambapo unatukumbusha kuhusu Moto na Pepo mpaka kama kwamba tunaviona. Lakini tunapoondoka basi tunachanganyikana na wake, watoto na wanyama ambapo tunasahau sana… “ Ndani yake imetajwa: “Ee Handhwalah! Mara hivi mara vile. Mara hivi mara vile. Mara hivi mara vile.”

Abu Sulaymaan ad-Daraaniy amesema:

“Hakika nafsi inapokuwa na njaa na kiu basi moyo unasafika na inaposhiba basi moyo unapofoka.”

[1] Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

al-Haakim pia ameisahihisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 15/05/2020