46. Yule mwenye kuwatukana Maswahabah ni mzushi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kumtukana mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamchukia kwa sababu ya kitu alichofanya au akayataja mabaya yake ni mtu wa Bid´ah mpaka awatakie rehema wote na asiwe na kinyongo na yeyote katika wao.”

MAELEZO

Hapa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ametaja kwamba yule mwenye kumchukia yeyote katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi anazingatiwa ni mtu wa Bid´ah. Kadhalika yule mwenye kutaja mabaya ya Swahabah; anazingatiwa pia kuwa ni mtu wa Bid´ah. Ataendelea kubaki katika hali hiyo mpaka awatakie rehema wote na moyo wake usiwe na kinyongo chochote dhidi yao. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewasifu na akawatapa katika Kitabu Chake. Hivyo basi, yule mwenye kuwatukana ameenda kinyume na Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Atakuja kupata malipo yake kwa sababu ya Bid´ah yake wakati atapokutana na Mola wake (Jalla wa ´Alaa).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau mmoja wenu atatoa dhahabu kiasi cha mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vilivyojazwa na mikono vya mmoja wao wala nusu yake.”[1]

Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah amepokea tawbah ya Nabii na Muhajiruun na Answaar ambao wamemfuata katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao zilikaribia kupondoka kisha akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[2]

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

[2] 09:117

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 159
  • Imechapishwa: 05/06/2019