46. Ufunguo wa maisha mazuri


Ninakhitimisha kwa nasaha ambayo inatakiwa kutendewa kazi na wanandoa wote. Jukumu kubwa lilioko kati ya wanandoa ni kusaidizana kujenga nyumba yenye dini na wote wawe na nia ya dini na wema. Kila mmoja amsaidie mwingine juu ya dini. Hilo linaleta raha, utulivu wa moyo na furaha nyumbani kwa njia isiyokuwa na kifani. Raha kubwa ilioko kwenye nyumba inatokamana na wanandoa kusaidizana juu ya kumtii Mola wa walimwengu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah Amrehemu mwanaume ambaye anaamka usiku kuswali na akamuamsha mke wake aswali. Akikataa anamnyunyizia maji usoni mpaka aamke na kuswali usiku. Allaah Amrehemu mwanamke ambaye anaamka usiku na kuswali na akamuamsha mume wake aswali. Akikataa anamnyunyizia maji usoni mpaka aamke na kuswali usiku.”[1]

Mume na mke wakisaidizana juu ya dini na kutekeleza dini ya Allaah nyumbani, basi wataishi nyumbani kwao maisha mazuri na yaliyo imara. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa nyumba ambayo Allaah Hutajwa na nyumba ambayo Allaah Hatajwi, ni kama mfano wa aliye hai na maiti.”[2]

Kukiwepo wema nyumbani basi ni lazima vilevile kupatikane furaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Furaha ya mwanaadamu iko katika mambo matatu na kutokuwa kwake na furaha kuko katika mambo matatu; miongoni mwa furaha ya mwanaadamu ni pamoja na kuwa na mwanamke mwema, kipando kizuri na nyumba pana. Kutokuwa na furaha kwa mwanaadamu kuko katika mambo matatu; nyumba mbaya, mwanamke mbaya na kipando kibaya.”[3]

Katika furaha ya mwanaadamu ni pamoja na nyumba yake iwe imejengwa juu ya wema. Hivyo basi, mcheni Allaah na saidizaneni na wake zenu juu ya dini na zijengeni nyumbani zenu katika dini. Kwa njia hiyo kuna uwezekano wa kila namna kuishi maisha mazuri:

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni muumini, Tutamhuisha maisha mazuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[4]

Allaah (´Azza wa Jall) Amemdhamini mume na mke maisha mazuri endapo watafanya matendo mema na kuamini. Hivyo basi, mcheni Allaah, waja wa Allaah, saidizaneni katika wema na uchaji Allaah na si katika madhambi na uadui.

Na Allaah ndiye Anajua zaidi. Allaah Amsifu Muhammad na kizazi chake.

[1] Abu Daawuud (1307), an-Nasaa’iy (1610), Ibn Maajah (1336), Ibn Khuzaymah (2/1148), Ibn Hibbaan (6/2567), al-Haakim (1/1164) na Ahmad (2/250). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim kutokamana na masharti ya Muslim na ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud (5/1181)).

[2] al-Bukhaariy (6407).

[3] Ibn Hibbaan (9/4033), al-Haakim (2/2640), Ahmad (1/168), at-Twayaalisiy (1/207) na wengine. Mnyororo wake ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim. Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy na al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (282).

[4] 16:97

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 24/03/2017