46. Sifa za sanda


41- Katika sanda kumependekezwa mambo yafuatayo:

La kwanza: Weupe. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Vaeni katika mavazi yenu yale meupe. Kwani hakika ndio bora ya mavazi yenu na wavikeni sanda ndani yake maiti zenu.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/176), at-Tirmidhiy (02/132) ambaye ameifanya kuwa Swahiyh, Ibn Maajah (01/449), al-Bayhaqiy (03/245), Ahmad (3426), adh-Dhwiyaa´ katika “al-Mukhtaarah” (02/229/60) kupitia kwa Ibn ´Abbaas. al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Mambo ni kama alivosema.

Vilevile ina Hadiyth nyingine yenye kuitolea ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Thamurah bin Jundub. Ameipokea an-Nasaa´iy (01/268), Ibn Jaaruud (260), al-Bayhaqiy (03/402-403) na wengineo.

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh pia kama alivosema al-Haakim, adh-Dhahabiy na al-Haafidhw katika “Fath-ul-Baariy” (03/105).

La pili: Sanda iwe mashuka matatu. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivikwa sanda kwenye mashuka matatu ya kiyemeni, meupepee na yanayotokana na pamba pasi na kanzu wala kilemba [alizungushiwa ndani yake].”

Wameipokea wasita, Ibn Jaaruud (259), al-Bayhaqiy (03/399), Ahmad (06/40, 93, 118, 165, 192, 203, 221, 231, 264) na ziada ni yake. Ndani yake kuna dalili ya wazi kwamba mashuka hayo hayakuwa yamedariziwa au kushonwa na wala hakukuwa na kanzu. Hadiyth iliopokelewa kuhusu jambo hilo ni Hadiyth munkari. Hayo yameyabainisha katika “adh-Dhwa´iyfah” (5909).

La tatu: Moja katika mashuka hayo liwe ni lenye misitarimisitari ikiwepesika kufanya hivo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapokufa mmoja wenu na akapata chochote, basi avikwe sanda ndani ya shuka moja yenye misitarimisitari.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/61), al-Bayhaqiy (03/403) kupitia njia yake, kupitia njia ya Wahb bin Munabbih kutoka kwa Jaabir kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Cheni ya wapokezi hii ni Swahiyh kwangu na vivyo hivyo kwa al-Mizziy. Ama al-Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw” (05/131):

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.”

Hadiyth hii ina njia nyingine kwa Ahmad (03/319), kutoka kwa Abu az-Zubayr, kutoka kwa Jaabir kwa tamko lisemalo:

“Yule atakayepata wasaa basi avikwe sanda kwenye shuka lenye michirizimichirizi.”

Tambua kwamba hakuna mgongano kati ya Hadiyth hii na ile Hadiyth ya kwanza inayozungumzia “weupe”:

“… na wavikeni sanda ndani yake maiti zenu.”

kwa sababu kuna uwezekano wa kuzioanisha kati yazo kwa njia miongoni mwa njia nyingi zinazotambulika kwa wanachuoni. Kinachoweza kunihudhurikia akilini mwangu ni njia mbili:

1- Shuka hilo liwe nyeupe lenye misitarimisitari na kilichochukuwa nafasi kubwa iwe ni weupe ikiwa sanda hiyo ni shuka moja. Katika hali hiyo Hadiyth ya pili itakuwa imekusanywa na ile Hadiyth ya kwanza kwa kuzingatia kwamba kila kitu huzingatiwa kile kilichochukua nafasi kubwa. Hapa ni pale ambapo sanda hiyo ni shuka moja. Ama mashuka yakiwa mengi basi kuoanisha kunakuwa kwepesi zaidi, nako ni njia inayofuatia:

2- Sanda moja ifanywe kuwa ni ile yenye misitarimisitari na zilizobaki ziwe nyeupe. Hapo Hadiyth zote mbili zitakuwa zimefanyiwa kazi. Haya ndiyo yamesemwa na Hanafiyyah kwa kutumia dalili ya Hadiyth hii. Haihusiani na ile Hadiyth ambayo al-Haafidhw ameinasibisha kwa Abu Daawuud, kutoka kwa Jaabir kwamba yeye (´alayhis-Salaam) alivikwa sanda mashuka mawili na shuka lenye misitarimisitari. Kisha akasema kuwa cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Hawakujenga hoja yao kwa Hadiyth hii. Bali haipatikani kwa Abu Daawuud. Bali inayopatikana kwake ni Hadiyth kutoka kwa ´Aaishah katika Hadiyth yake, nayo ni ile ya pili ambayo alisimulia: “Kuliletwa kipande cha shuka lakini akairudisha nyuma na wala hawakumkafini ndani yake.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh lau si kusimulia Abu az-Zubayr kwa kutotaja majina. Lakini inasihi kutokana na ya kabla yake.

La nne: Kuifukiza udi/ubani  mara tatu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pindi mtapomfukiza maiti basi mfukizeni mara tatu.”

Ameipokea Ahmad (03/331), Ibn Abiy Shaybah (04/92), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (752- al-Mawaarid), al-Haakim (01/355) na al-Bayhaqiy (03/405). al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.  Mambo ni kama alivosema. Ameisahihisha an-Nawawiy pia katika “al-Majmuu´” (05/196).

Hukumu hii haimkusanyi Muhrim. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya yule Muhrim ambaye alivunjwa shingo yake na mnyama wake:

“… na wala msimtie manukato.. “

Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake pamoja na daraja yake katika masuala ya 17 nambari. 8 ukurasa wa 52-53.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 82-84
  • Imechapishwa: 26/02/2020