Baada ya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza kisomo alikuwa akinyamaza kidogo[1]. Halafu akiinyanyua mikono yake[2] kama alivyofanya katika Takbiyrat-ul-Ihraam, analeta Takbiyr[3] na kwenda katika Rukuu´[4]. Hivyo ndivyo alivyomwamrisha yule aliyeswali kimakosa na kumwambia:

“Hakika haitimii swalah ya mmoja wenu mpaka atawadhe vizuri kama alivyomwamrisha… Halafu amtukuze Allaah, amuhimidi na amsifu, asome kile akiwezacho katika Qur-aan katika yale aliyomfunza Allaah, aseme Takbiyr, aende katika Rukuu´ na aiweke mikono yake kwenye magoti yake mpaka viungo vyake vyote vitulie na vipumzike… “[5]

[1] Abu Daawuud na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Kwa mujibu wa Ibn-ul-Qayyim na wengineo kipindi hichi kifupi ni kwa ajili ya kuvuta pumzi.

[2] al-Bukhaariy na Muslim. Kitendo hichi kimepokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika inahusu kunyanyua mikono baada ya Rukuu´. Haya ndio maoni ya wale maimamu watatu na wengi katika Muhaddithuun na Fuqahaa´. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) alikuwa na maoni haya wakati alipokufa, kama alivyopokea Ibn ´Asaakir (2/78/15). Vilevile baadhi ya Hanafiyyah wana maoni haya. Miongoni mwao ni Iyswaam bin Yuusuf ambaye alikuwa mwanafunzi wa Abu Uswmah al-Balkhiy (aliyefariki. 210) ambaye na yeye alikuwa mwanaunzi wa Imaam Abu Yuusuf (Rahimahu Allaah). Haya tayari yameshatajwa katika utangulizi. ´Abdullaah bin Ahmad amesema katika “al-Masaa-iyl” yake kwamba baba yake amesema:

“Imepokelewa kutoka kwa ´Uqbah bin ´Aamir ya kwamba amesema kuhusiana na kunyanyua mikono katika swalah: “Anapata thawabu kumi kila anaponyanyua.” (Uk. 60)

Imekuja katika Hadiyth Qudsiy:

“Yule mwenye kunuia kufanya tendo jema na akakitekeleza basi Allaah atamwandikia mema kumi hadi mia saba.” (Swahiyh-ut-Targhiyb (16))

[3] al-Bukhaariy na Muslim.

[4] al-Bukhaariy na Muslim.

[5] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy. al-Haakim ameisahihsiha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 112
  • Imechapishwa: 17/02/2017