1 – Abu Hurayrah amesimulia:

“Kulisemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni watu gani watukufu zaidi?” Akasema: “Watukufu zaidi mbele ya Allaah ni wale wachaji Allaah zaidi.” Wakasema: “Hatukuulizi juu ya hilo.” Akasema: “Mnaniuliza kuhusu asili ya waarabu?” Wakaitikia: “Ndio.” Akasema: “Mbora wenu katika kile kipindi cha kikafiri ndiye mbora wenu katika Uislamu wakiwa na ufahamu.”

2 – Watu bora ni wale wenye kumcha Allaah zaidi. Mtukufu ni mchaji. Kumcha Allaah ni kule kuazimia kutekeleza yale yaliyoamrishwa na kuepuka yale yote yaliyoharamishwa. Yule ambaye ana maazimio kikweli juu ya sifa mbili hizi basi ni mchaji Allaah ambaye anastahiki kuitwa “mtukufu”. Ambaye ataacha mawili hayo au moja wapo au kitu katika viwili hivyo basi amekosa utukufu wake kwa mujibu wa kile kilichokosekana.

3 – Mtukufu hawi mwenye chuki wala mwenye hasadi. Hawi na furaha ya kiadui. Hawashambulii wengine. Hajishughulishi na mambo ya kipuuzi. Si mwenye kufanya madhambi mazito. Si mwenye kujifakhari. Si mwongo. Si mwenye kuchoka haraka. Hakati mafungamano na rafiki yake. Hawaudhi ndugu zake. Hapotezi kile ambacho ana jukumu juu yake. Hakiuki katika mapenzi. Anampa yule ambaye hatarajii huduma kutoka kwake. Anampa amani yule asiyeogopa. Anasamehe wakati anaweza kuadhibu. Anaunga wale waliomkata.

4 – Ibraahiym bin Shkilah amesema:

“Hakika kila kitu kina uhai na kifo. Kuwa na mawasiliano na watukufu kunahuisha utukufu. Kutangamana na waovu kunahuisha uovu.”

5 – Mtukufu anakuwa mlaini pindi anapofanyiwa huruma. Mbaya anakuwa mgumu zaidi pindi anapofanyiwa upole. Mtukufu anawatukuza watukufu. Hawatwezi wabaya. Hamuudhi mwenye busara. Hamchezei shere mpumbavu. Hatangamani na mtu mwenye madhambi mazito. Anawapendelea ndugu zake mbele ya nafsi yake. Anawapa kile anachomiliki.

6 – Ibraahiym bin Abiy ´Aliyyah amesema:

“Nilimuona Saalim bin ´Abdillaah na Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz wakipanda mnyama kuelekea nchi ya warumi. Pindi mnyama wa mmoja wao anapopumzika, basi husimama mwengine ili yule mwengine aweze kumuwahi.”

7 – ash-Sha´biy amesema:

“Watukufu zaidi wa watu ni wale wenye kupenda haraka na kuchukia taratibu. Wamefanana na kikombe cha fedha kinachovunjika taratibu na kutengenezwa haraka. Wabaya zaidi wa watu ni wale wenye kupenda taratibu na kuchukia haraka. Wamefanana na kikombe cha udongo kinachovunjika haraka na kutengenezwa taratibu.

8 – Mtukufu hushukuru pale anapopewa. Anampa udhuru yule mwenye kumnyima. Anamuunga yule mwenye kumkata. Anamfadhilisha yule mwenye kumpa. Anampa yule mwenye kumuomba. Huchukua hatua ya kumpa yule asiyemuomba. Anamuhurumia mnyonge. Pindi mtu anapomuona kuwa ni mnyonge, basi huona kifo ni kitukufu zaidi kuliko kuonekana hivo. Mbaya ni yule ambaye yuko kinyume kabisa na yale yote tuliyotaja.

9 – Abu ´Iysaa amesema:

“Ibraahiym bin Adham alikuwa mtukufu. Alikuwa akitangamana na watu kwa tabia zao kama walivyo. Wakati mwingine aliwaalika kwenye nyama za kuchomwa na tende. Wakati mwingine inatokea anapokuwa peke yake na  marafiki zake anaoanasika nao basi hugombana. Alikuwa akifanya kazi za wanamme wawili. Hata hivyo anapokuwa mwenyewe basi hula unga.

10 –  Abul-Hawaariy amesema:

“Hakuna mtu yeyote isipokuwa tawbah yake ni yenye kukubaliwa. Isipokuwa yule mtu mwenye tabia mbaya. Hakuna dhambi anayotubia kwayo isipokuwa anaingia ndani ya nyingine ambayo ni mbaya zaidi.”

11 – Mtu mtukufu huacha athari yenye kusifiwa duniani. Matendo yake ni yenye kuridhiwa huko Aakhirah. Anapendwa na kila mtu. Mwenye kuridhika na asiyeridhika anafahamiana naye. Adui na mnyonge anajitenga naye mbali. Mwenye busara na mtukufu anasuhubiana naye.

12 – Sijaona kitu kinachopunguza utukufu wa mtukufu kama ufukara ni mamoja uko moyoni au kwenye kitu.

13 – Abu Juhayfah amesema:

“Keti na wakubwa. Tangamana na wenye hekima. Waulize wanazuoni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 171-176
  • Imechapishwa: 14/08/2021