46. Maovu ya sita: Pete ya uchumba


06- Pete ya uchumba

Jambo la sita: Baadhi ya wanaume kuvaa pete ya dhahabu wanayoiita “pete ya uchumba”. Hili pamoja na kuwa ndani yake kuna kujifananisha na makafiri vilevile – kwani desturi hii imetuingilia kutoka kwa manaswara – ndani yake pia kuna kwenda kinyume waziwazi na maandiko sahihi ambayo yanaharamisha dhahabu kwa wanaume na kwa wanawake pia, kama utavopata kujua hilo. Yafuatayo ni baadhi ya hayo maandiko:

La kwanza: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza pete ya dhahabu.”[1]

La pili: Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona pete ya dhahabu kwenye mkono wa mwanamume mmoja ambapo akaitoa na kuitupa na kusema: “Hivi kweli mmoja wenu anakusudia kuchukua kaa la moto na kuliweka mkononi mwake?” Baada ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameshaenda mtu yule akaambiwa: “Chukua pete yako na unufaike nayo!” Akasema: “Hapana, ninaapa kwa Allaah sintoichukua ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameshaitupa.”[2]

La tatu:  Abu Tha´labah al-Khushaniy amesimulia ya kwmaba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona pete ya dhahabu mkononi mwake ambapo akawa anaipiga kwa kijiti alichokuwa nacho. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa amezubaa kidogo akaitupa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaitazama na hakuiona tena kwenye mkono wake. Akasema: “Hukuitupa isipokuwa baada ya kukuumiza na kukupatia maumivu.”[3]

La nne: ´Abdullaah bin ´Amr ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Swahabah mmoja amevaa pete ya dhahabu ambapo akawa amempa mgongo. Swahabah yule akaitupa na akachukua pete ya chuma. Mtume akasema: “Hii ni mbaya zaidi. Kwani hili ni pambo la watu wa Motoni.” Hivyo Swahabah yule akawa ameitupa na akachukua pete ya fedha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema kitu kwayo.”[4]

La tano: “Yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho, basi asivae hariri wala dhahabu.”[5]

La sita: “Atakayevaa dhahabu katika Ummah wangu kisha akafa ilihali bado ni mwenye kuivaa, basi Allaah atamharamishia dhahabu ya Peponi.”[6]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (10/259), Muslim (06/135), Ahmad (04/287) kutoka kwa al-Baraa´ bin ´Aazib, al-Bukhaariy (10/260), Muslim (06/149), an-Nasaa´iy (02/288), Ahmad (02/468), Ibn Sa´d (01/02/161) kutoka kwa Abu Hurayrah. Katika mlango huo amepokea vilevile ´Aliy, ´Imraan na wengineo.

[2] Ameipokea Muslim (06/149), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (01/150), at-Twabaraaniy (01/150/02-03), Ibn ad-Diybaajiy katika “al-Fawaa-id al-Muntaqaah” (01/80/02-02).

[3] Ameipokea an-Nasaa´iy (02/288), Ahmad (04/195), Ibn Sa´d (07/416), Abu Nu´aym katika “Aswbahaaniy” (01/400) kutoka kwa an-Nu´maan bin Rashiyd, kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa ´Atwaa´ bin Yaziyd, kutoka kwa Tha´labah.

[4] Ameipokea Ahmad (6518) na (6680), al-Bukhaariy katika “Aadab-ul-Mufrad” (1021) kutoka kwa ´Amr bin Shu´ayb, kutoka kwa baba yake. Mlolongo wa wapokezi ni mzuri. Ibn Rajab ameinyamazia katika “Sharh at-Tirmidhiy” (02/90).

[5] Ameipokea Ahmad (05/261) kutoka kwa Abu Umaamah ambaye amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

[6] Ameipokea Ahmad (6556) na (6947) kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr ambaye ameipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Muheshimiwa Shaykh Ahmad Muhammad Shaakir ameizungumzia katika taaliki yake juu ya “al-Musnad”. Amefanya vizuri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 212-222
  • Imechapishwa: 02/05/2018