46. Kuitwa “qaadhi wa maqaadhi” na mfano wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Imesihi kupokelewa kupita kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jina twevu na lenye kuchukiza mbele ya Allaah ni mtu kujiita “mfalme wa wafalme”. Hakika hakuna mfalme isipokuwa Allaah.”[1]

Sufyaan amesema:

“Mfano mwingine ni kama mtu kujiita “Shaahaan Shaah”.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mtu anayechukiwa zaidi na Allaah siku ya Qiyaamah na mbaya zaidi… “[2]

Mtwevu bi maana mbaya.

MAELEZO

Alichokusudia mwandishi kwa kichwa cha khabari hiki ni makatazo juu ya majina yanayoweza kufanana na majina ya Allaah. Kwa sababu Yeye (Subhaanah) ana majina ambayo amepwekeka nayo. Baadhi ya majina hayo ni ”ar-Rahmaan”, ”Maalik-ul-Mulk”, ”al-Khallaaq”, ”Rabb-ul-´Aalamiyn”, ”Haakim-ul-Hukkaam”na ”Sultwaan-us-Salaatwiyn”. Katika kuikamilisha na kuitimiliza Tawhiyd ni kujiepusha kujiita majina kama haya. Kujiita majina kama hayo ni jambo linaipunguza Tawhiyd na imani. Haijuzu.

Kadhalika inahusiana na “qaadhiy wa maqaadhiy”. Hili ni jambo lipo katika baadhi ya miji. Hata kama wanamaanisha kwamba mtu huyo ndiye hakimu wa mahakimu katika nchi hiyo lakini hata hivyo ni jina lisilosilihi na lisilofaa.

Ama ikiwa jina hilo litafungamanishwa na nchi fulani kama kwa mfano “qaadhiy wa maqaadhiy wa Misri au Makkah” ni jambo linakuwa na wepesi fulani, lakini pamoja na hivyo kuacha kufanya hivo ndio bora zaidi. Badala yake mtu anaweza kutumia jina “kiongozi wa maqaadhiy” au “amiri wa maqaadhiy” ili mtu awe ameepuka majina haya yanayotajwa kwa kutokufungamanisha.

1- Imesihi kupokelewa kupita kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jina twevu na lenye kuchukiza mbele ya Allaah ni mtu kujiita “mfalme wa wafalme”. Hakika hakuna mfalme isipokuwa Allaah.”

Bi maana jina dhalili na lenye kuchukiwa zaidi.

 Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza jina hilo kwa sababu linamfanya mtu kufikiria sifa isiyoendana naye. Sifa kama hiyo ni ya Allaah (Ta´ala) peke yake. Mtu sio mfalme wa wafalme. Si jina lenye kusilihi kwake. Vivyo hivyo inahusiana na majina mengine yote.

Shaahaan Shaah ni jina la wasiokuwa waarabu na maana yake ni “mfalme wa wafalme”.

[1] al-Bukhaariy (6205) na Muslim (2143).

[2] Muslim (2143).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 141
  • Imechapishwa: 03/11/2018