46. Hizbiyyuun wao wenyewe hawahukumu kwa Shari´ah ya Allaah


Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wana wa israaiyl walikuwa wakiongozwa na Mitume. Kila ambapo Mtume anapokufa basi anachukua nafasi yake Mtume mwingine. Hakuna Mtume mwingine baada yangu lakini hata hivyo watakuwepo makhaliyfah wengi.” Wakasema: “Unatuamrisha nini?” Akasema: “Timizeni kiapo kimoja baada ya kingine na wapeni haki zao. Hakika Allaah atawauliza yale aliyowachungisha.”[1]

Hakusema kwamba sisi ndio tuwafanyie hesabu, tuwafanyie mapinduzi, tuwafanyie uasi au tuchukue haki zetu. Baadhi ya wafanya mapinduzi wakubwa wanasema kuwa hawasubiri suluhu itayotoka kutoka mbinguni na kwamba ni lazima wachukue haki zao kwa mikono yao na wanawashaji´isha umati wa watu hali kadhalika. Hawafanyi hivo kwa kuwa na ghera juu ya dini ya Allaah wala juu ya Ummah. Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mtu aliyekuwa na ghera zaidi. Katika mnasaba mmoja Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) alisema:

“Unaonaje lau nitamkuta mwanaume na mke wangu na kuleta mashahidi wane?” Ninaapa kwa Allaah ya kwamba nitamdunga ncha ya mkuki.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hivi mnashangazwa na wivu wa Sa´d? Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mimi nina wivu zaidi yake na Allaah ana wivu zaidi yangu. Kwa ajili hiyo ndio maana ameharamisha machafu.”[2]

Pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… wapeni haki zao. Hakika Allaah atawauliza yale aliyowachungisha.”

Sio wewe utakayemfanyia hesabu kiongozi. Badala yake unatakiwa kumnasihi. Akisikiza ni vizuri na la sivyo umeshatekeleza wajibu wako. Ni lazima kwako kusubiri midhali anaswali. Haya si maneno yetu wenyewe. Lakini hata hivyo yanachoma na yanaumiza kuyasikia:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao kisha wasipate katika nyoyo zao kipingamizi katika yale uliyohukumu na wajisalimishe ukweli wa kujisalimisha.”[3]

Wanaita Haakimiyyah lakini wao wenyewe hawahukumu kwa Allaah wala kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ahl-ul-Bid´ah wanaamini Wahdat-ul-Wujuud, wanaukafirisha Ummah na wanaona kuwa Qur-aan imeumbwa. Hawahukumu kwa Shari´ah ya Allaah. Hawako radhi kuhukumiwa kwa Shari´ah ya Allaah katika mambo kama haya. Ni watu wako mbali kabisa na hukumu ya Allaah. Wanaita katika hukumu ya Allaah ilihali wao wenyewe ni miongoni mwa wafanya ghasia wakubwa kabisa dhidi ya hukumu ya Allaah na kurudi kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Je, Hadiyth hizi ni mchezo? Wanaonelea kuwa Hadiyth hizi ni kuwasapoti makafiri na wakanamungu.

[1] al-Bukhaariy (3455) na Muslim (1842).

[2] al-Bukhaariy (7416) na Muslim (1499).

[3] 04:65

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 417-418
  • Imechapishwa: 23/10/2017