Miongoni mwa hekima ya funga ni kwamba ni sababu ya kumcha Allaah. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[1]

Mfungaji ameamrishwa kufanya matendo mema na kujiepusha na matendo maovu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Ikiwa mfungaji ni mwenye kubabaika wakati wa funga basi kila ambapo atatamani kufanya maasi basi anakumbuka kuwa amefunga na hivyo anajizuia nayo. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwamrisha mfungaji kumjibu yule mwenye kumtukana:

“Hakika mimi nimefunga.”

Huko ni kumzindua juu ya kwamba mfungaji ameamrishwa kujizuia kutukanana. Pia anaikumbusha nafsi yake kuwa amefunga na hivyo akajizuia kumkabili kwa matusi.

[1] 02:183

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 64
  • Imechapishwa: 14/05/2020